Tiba mkoba yamuwezesha kupata huduma za kibingwa JKCI
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa tundu dogo kwa kutumia mtambo wa cathlab
kumuwekea kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker). Mgonjwa
huyo alifanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyofanyika
Mkoani Kagera wiki iliyopita.
Daktari bingwa wa moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye akimuwekea mgonjwa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya kazi vizuri (Pacemaker) kwa kutumia mtambo wa Cathlab. Mgonjwa huyo alifanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo iliyofanyika Mkoani Kagera wiki iliyopita.
********************************************************************************************
Mgonjwa aliyefanyiwa uchunguzi katika kambi maalumu ya
matibabu ya moyo iliyofanyika mkoani Kagera wiki iliyopita awekewa kifaa cha kuusaidia
moyo kufanya kazi vizuri “Pacemaker”.
Mgonjwa huyo alikuwa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo
hivyo mapigo yake ya moyo kuwa chini ya 50 na kupata changamoto za kizunguzungu
na wakati mwingine kupoteza fahamu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo na mfumo wa umeme wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Yona Gandye alisema baada ya mgonjwa huyo kufanyiwa uchunguzi katika
kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan outreach services iliyofanyika
mkoani Kagera na kugundulika kuwa na tatizo la mfumo wa umeme wa moyo alipewa
rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi.
Dkt. Gandye alisema mgonjwa huyo amechuka hatua za haraka
kufika ambapo amefanyiwa uchunguzi zaidi na baadaye kufanyiwa upasuaji mdogo wa
moyo kwa kutumia mtambo wa cathlab kuwekewa kifaa cha kuusaidia moyo kufanya
kazi vizuri (Pacemaker).
“Kikawaida mapigo ya moyo yanatakiwa kuanzia 50 hadi 100 kwa
dakika moja, mgonjwa huyu mapigo yake yalikuwa chini ya 50 lakini baada ya
matibabu mapigo yake yamekuwa yakawaida”, alisema Dkt. Gandye
Dkt. Gandye alisema baada ya kumalizika kwa kambi hiyo ijumaa
ya wiki iliyopita hadi sasa wagonjwa watatu kati ya 55 waliopewa rufaa kufika
JKCI kwaajili ya matibabu zaidi wamefika na kupatiwa huduma.
Kwa upande wake mgonjwa kutoka Kagera AnaJoyce Laurent
alisema hakuwahi kujua kama na tatizo la shinikizo la juu la damu na matatizo
ya mfumo wa umeme wa moyo hadi hapo alipofika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba
(BRRH) wiki moja kabla ya kambi maalumu ya matibabu ya moyo akiwa na tatizo la
kichomi.
AnaJoyce alisema baada ya kufanyiwa uchunguzi wataalamu wa
afya wa BRRH walimshauri kufika katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo
iliyokuwa ikiendeshwa na JKCI kuonana na daktari bingwa wa moyo kutokana na
mapigo yake ya moyo kuwa chini ya 50.
“Nilifuata ushauri wa madaktari na kuonana na bingwa wa moyo
wa JKCI jumatatu iliyopita wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya moyo ambaye
alinishauri kufika JKCI mapema kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo kuwekewa kifaa cha
kuusaidia moyo kufanya kazi, nimeshafanyiwa upasuaji na kuwekewa kifaa hicho na
sasa naendelea vizuri”, alisema AnaJoyce.
AnaJoyce aliwashukuru wataalamu wa afya wa JKCI kwa kumpatia
matibabu kwa haraka na kuwapongeza wataalamu hao kwa kazi nzuri wanayofanya ya
kuokoa maisha ya wagonjwa.
Comments
Post a Comment