RC Mwasa: Wananchi Kagera changamkieni fursa ya kupima moyo
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajati Fatma Mwasa akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa watu 288 wameshapata huduma za matibabu.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye akizungumza na wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo ambapo hadi sasa watu 288 wameshapata huduma za matibabu.
Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera wakimsikiliza mkuu wa mkoa huo Mhe. Hajati Fatma Mwasa wakati wa ufunguzi wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH).
Wananchi wa Mkoa wa Kagera wamehimizwa
kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH) kwa ajili ya kupimwa na
kutibiwa magonjwa ya moyo kutokana na uwepo wa kambi maalumu ya matibabu inayoendeshwa
na madaktari bingwa wa magojwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo na mkuu wa
mkoa huo Mhe. Hajati Fatma Mwasa wakati akifungua kambi hiyo ya kibingwa ya
siku tano amabapo wananchi wanapata huduma za kibingwa ikiwa ni pamoja na kipimo
cha kuangalia moyo unavyofanya kazi, kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa
moyo, elimu ya lishe bora na matumizi sahihi ya dawa za moyo.
Mhe. Hajati Mwasa alisema kuna kila
sababu ya kuendelea kumshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa
aliyoifanya ya kuboresha sekta ya afya katika mkoa wa Kagera kwa kupeleka mashine mpya na za kisasa
zinazotusaidia wananchi kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.,
Bukoba.
“Mashine zilizopo zimewasaidia pia wataalamu
wa JKCI kutoa huduza za uchunguzi kwa urahisi kwani vifaa wamevikuta hapa na
vingine wamekuja navyo, hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Kagera
kuendelea kufika hapa hospitali kufanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo na kujua
hali zenu”, alisema Mhe.Hajati Mwasa.
Aidha, ameupongeza na kuushukuru uongozi
pamoja na madakatari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kufika katika mkoa wa Kagera ili kutoa huduma za vipimo mbalimbali vya magonjwa
ya moyo huku akiwasihi kuendelea kuutembelea mkoa huo mara kwa mara na kuwasaidia
wananchi kupata huduma hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, daktari bingwa
wa magonjwa ya moyo kutoka JKCI Yona Gandye aliushukuru uongozi wa mkoa wa
Kagera kwa kuwapokea na kuwakubalia kutoa huduma ya uchunguzi na matibabu ya
moyo kwa wananchi.
Dkt. Gandye alisema JKCI imekuwa na
utaratibu wa kuwafauata wananchi mahali walipo na kutoa huduma ya tiba mkoba ijulikanayo
kwa jina la Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan
Outreach Services ambayo imewezesha kuwafikia wananchi wengi na kupata huduma za
matibabu kwa wakati tofauti na ambavyo wangezifuata huduma hizo JKCI.
“Tangu tumeanza kutoa huduma hizi
tumeshafika katika mikoa 12 ya Tanzania bara na Visiwani na huu ni mkoa wa 13,
tumeshafanya upimaji wa aina hii katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Geita,
Mtwara, Lindi, Dodoma, Iringa, Manyara,Kilimanjaro na Visiwa vya Unguja na
Pemba”.
“Wananchi 10,807 walifanyiwa vipimo
kati ya hao 4375 walikutwa na magonjwa mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la
juu la damu (BP), kutanuka kwa misuli ya moyo, kuziba kwa mishipa ya damu ya
moyo, matundu kwenye moyo, valvu za moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokukaa
katika mpangilio wake. Wagonjwa 1323 tuliwapa rufaa ya kuja kutibiwa katika
Taasisi yetu na tayari wengine wameshakuja na kupatiwa matibabu ya kibingwa”,
alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dkt. Museleta Nyakiroto alimshukuru mkuu wa mkoa
wa Kagera Hajati Fatma Mwasa kwa kufungua kambi hiyo ya utoaji wa huduma za
kibingwa huku akisisitiza kuwa lengo la
kambi hiyo ni kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuwapunguzia adha ya
kufuata huduma hizo katika mikoa ya mbali ukiwemo mkoa wa Dar es Salaam na
Mwanza.
Dkt. Museleta Nyakiroto alisema
katika kambi hiyo wananchi wanapata huduma zote za vipimo ya mayo huku
akisisitiza kuwa mnamo mwezi Aprili 08, 2024 wanategemea kuwa na kambi nyingine
ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Kanda ya Bugando watakaokuja kutoa
huduma kwa watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Comments
Post a Comment