Mashabiki wa Arsenal Afrika watoa msaada wa milioni 16 na kuchangia damu JKCI
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal Afrika pamoja na wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 16 iliyotolewa na mashabiki hao kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na kutoa damu kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa upasuaji.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Teknolojia na Kilimo cha Jomo Kenyatta kilichopo nchini Kenya ambaye pia ni Afisa Uuguzi Tonny Mbaja akimpima shinikizo la damu shabiki mwenzake wa Arsenal Afrika wakati mashabiki wa timu hiyo walipofika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na kutoa damu kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa upasuaji.
Mteknolojia wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Chuvaka akimfanyia usajili kabla ya kuchangia damu shabiki wa Arsenal Afrika wakati mashabiki wa timu hiyo walipofika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na kutoa damu kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa upasuaji.
*****************************************************************************************************************************************************************************
Mashabiki wa Arsenal Afrika wametoa msaada wa shilingi
milioni 16 pamoja na kuchangia damu kwa ajili ya watoto wanaofanyiwa upasuaji
wa moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Akipokea msaada huo leo jijini Dar es Salaam Mkuu wa Wilaya
ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo aliwashukuru mashabiki wa timu hiyo na kusema kuwa
fedha walizozitoa pamoja na damu waliyochangia
itasaidia kuokoa maisha ya watoto wenye
matatizo ya moyo.
Mhe. Mpogolo aliwaomba wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada
zinazofanywa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) za kuhakikisha watanzania wanapata matibabu bora ya moyo kwa kuchangia
gharama za matibabu kwa watu wasiokuwa na uwezo wakiwemo watoto ambao wako zaidi
ya 600 wanasubiri kufanyiwa upasaji.
“Tumeambiwa wagonjwa zaidi ya 6000 wanafanyiwa upasuaji wa moyo
robo tatu ya wagonjwa hawa ni watoto, Serikali imebeba jukumu la kumtibu mtoto
kwani mzazi anapofika JKCI na kutambua mtoto wake ana shida ya moyo anakuwa tayari
ametumia fedha nyingi na hivyo wengine kukosa kabisa fedha za kulipia gharama za
matibabu”.
“Gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto ni milioni nane hadi
10 Serikali inagharamia matibabu haya kwa zaidi ya asilimia 70 na wakati mwingine kwa asilimia 100. Ninawashukuru sana
washabiki wa Arsenal kwa kuiunga mkono Serikali na kuwasaidia watoto wenye
uhitaji wamefanya matendo ya huruma kwa kuwakumbuka wasio na uwezo”, alisema
Mhe. Mpogolo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kutokana na uwekezaji mkubwa
uliofanywa na serikali wa kusomesha wataalamu pamoja na kununua vifaa tiba vya
kisasa ambao umeiwezesha JKCI kutoa huduma bora za matibabu ya moyo barani
Afrika ndiyo maana washabiki wa timu ya Arsenal Afrika wakaona wawatembelee na
kutoa msaada kwa watoto.
“Mashabiki wa Arsenal Afrika wametutembelea wametoa mchango
wa fedha za upasuaji wa moyo kwa watoto pamoja na kuchangia damu, mchango huu
ni mkubwa kwani kufika kwa mashabiki hawa hapa JKCI kutatangaza utalii tiba na
kuifanya Taasisi yetu kuendelea kutambulika kimataifa”.
“Ninawaomba wananchi wafanye mazoezi kwa kushiriki michezo
mbalimbali kwani magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yakiwemo ya yanaongezeka kwa kasi ni muhimu kufanya mazoezi ili kujikinga na
magonjwa haya pia niniomba wananchi wajenge tabia ya kuisaidia jamii inayowazunguka”,
alisema Dkt. Kisenge.
Naye katibu wa Arsenal Tanzania Mboka Francis alisema mwaka
2012 mashabiki wa timu hiyo hapa nchini walianza kukutana na kufanya shughuli
mbalimbali na ilipofika mwaka 2014 wakatambulika Arsenal London .
“Miaka ya nyuma tulikuwa tukikutana tunaangalia mpira wa
Arsenal na kujadili maendeleo ya timu yetu, baadaye tukaona tufanye kitu cha kuisaidia
jamii inayotuzunguka ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Unaweza kuona
mchango tulioutoa ni mdogo lakini tunafanya hivi kwa kuihamasisha jamii ifanye vitu
kama hivi na kuiokoa jamii yao inayowazunguka”, alisema Francis.
Nao mashabiki wa Arsenal Afrika walisema wamekuwa na tabia ya
kukutana kila mwaka katika nchi watakayoichagua kwa ajili ya kubadilishana
mawazo na kuchangia jamii inayowazunguka.
“Tumewapokea wenzetu kutoka nchi mbalimbali za Afrika, tumekuwa
na ushirikiano mkubwa sisi tuko sehemu
ya jamii hivyo basi furaha ya kushabikia timu yetu tuliyokuwa nayo tunatakiwa kuishirikisha
jamii ndiyo maana tunawasaidia watu wasiokuwa na uwezo ili nao wapate furaha”.
“Ukiwa shabiki wa michezo uwe zaidi ya michezo na kuendeleza undugu kwa
kuwashika wengine mkono na kugusa maisha yao”, alisema Steven Matinya shabiki
wa Arsenal Tanzania.
“Licha ya kuichangia
fedha timu yetu ya Arsenal, kila mwaka tunaungana kutoka nchi mbalimbali Afrika
tukiwa na lengo moja la kurudisha kwa
jamii kile tulichokuwa nacho kwa kuwasaidia watu wasio na uwezo, tunafanya utalii
na tunachangia damu kwa ajili ya wagonjwa”, alisema Peter Mzembi kutoka tawi la
Arsenal Kericho Kenya.
Kila mwaka mashabiki wa timu hiyo kutoka nchi mbalimbali Afrika wanakutana katika nchi watakayoichagua kwa ajili ya kufanya tamasha la kubadilishana mawazo mbalimbali pamoja na kufanya tukio la hisani la kuchangia wahitaji.Kwa mwaka huu mashabiki hao wapatao 361 kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia na Zambia wamekutana jijini Dar es Salaam Tanzania.
Comments
Post a Comment