Dar kupimwa moyo Machi 2 & 3, 2024
Mwakilishi wa umoja wa wanawake Hospitali ya JKCI Dar Group Debora Mkemwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tiba mkoba itakayofanyika tarehe 2 na 3 Machi 2024 katika viwanja vya Hospitali hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Picha na: Khamis Mussa
*************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group
kuadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kufanya kambi maalumu ya upimaji na
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi.
Kambi hiyo ya siku mbili itafanyika katika viwanja vya
Hospitali ya JKCI Dar Group tarehe 2 na 3 Machi 2024 kwa kufanya uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu
Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group Idd Lemmah alisema upimaji huo
unafanyika kupitia kambi maalumu ijulikanayo kama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
tiba mkoba iliyolenga kuwafikishia watanzania huduma za matibabu karibu.
“Tunawakaribisha watanzania mjitokeza, hususani watu
wanaoizunguka Hospitali hii wa Tazara na Temeke mfike katika siku hizi mbili
mchunguze afya zenu”, alisema Lemmah
Kwa upande wake Kaimu mkuu wa huduma za tiba wa Hospitali ya JKCI
Dar Group Dkt. Eva Wakuganda alisema kupitia kambi hiyo wananchi watapata fursa
ya kutibiwa na wataalamu wa afya mabingwa wa magonjwa ya moyo.
Dkt. Eva ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa
watoto alisema wanawake wa JKCI Dar Group wameona umuhimu wa kuadhimisha siku
ya wanawake duniani kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwasababu wagonjwa wengi
wamekuwa wakichelewa kufika hospitali kwaajili ya kupata matibabu.
“Kila watoto 100 wanaozaliwa mtoto mmoja uzaliwa na magonjwa
ya moyo lakini bahati mbaya hawafiki hospitali mapema kwaajili ya kupatiwa
matibabu hivyo kupitia kambi zetu za matibabu tunawatambua mapema na kuwapa
huduma mapema”, alisema Dkt. Eva
Dkt. Eva alisema kupitia kambi hiyo wananchi hupata elimu ya
lishe na elimu ya kutambua magonjwa ya moyo hivyo kuwapa nafasi kujilinda na
magonjwa hayo na pale wanapoyapata kuweza kuona dalili zake mapema hivyo kuwahi
hospitali.
“Dalili za magonjwa ya moyo kwa watoto ni pamoja na
kubadilika rangi kuwa wa bluu kwenye midomo na vidole, kushindwa kupumua
vizuri, kutokuongezeka uzito, mapigo ya moyo kwenda mbio, kuchoka na kutokwa na
jasho mara kwa mara”, alisema Dkt. Eva
Naye mwakilishi wa umoja wa wanawake Hospitali ya JKCI Dar
Group Debora Mkemwa alisema wanawake wa Hospitali hiyo wameona umuhimu wa
kuadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa
wananchi kwani wanawake ndio nguzo ya kujenga familia bora.
“Wanawake ni msingi wa kuhakikisha familia zetu zinakuwa bora
na imara kama ambavyo kauli mbiu ya siku ya wanawake duniani ya mwaka huu
inavyosema ‘Wekeza kwa wanawake kwaajili
ya maendeleo endelevu”,alisema Debora
Debora alisema wanawake watakapofikiwa na taarifa za upimaji
huo watoe taarifa ndani ya familia zao, kuwahamasisha watu waliopo katika
familia zao ili kwapamoja waweza kupata fursa ya kupima moyo.
“Kambi kama hizi zinapofanyika zinampa mwananchi fursa ya
kujijua, kupata matibabu kwa wakati, kwa muda mfupi na kwa gharama nafuu
tofauti na mtu anayefika hospitali kwa kuchelewa”, alisema Debora
Comments
Post a Comment