Wafurahia kufanyiwa ECHO na ECG bila malipo
Mtaalamu wa afya kutoka Shirika la Cardiostart International
la nchini Marekani Savannah Breaker pamoja na madaktari wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete Hospitali ya Dar Group Samweli Mbilinyi na Masanja James
wakijadiliana baada ya kumfanyia mgonjwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa
moyo (ECG) wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya kufanya vipimo vya moyo kwa
wananchi wa Dar es Salaam bila malipo iliyofanyika katika Hospitali ya JKCI Dar
Group.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya Dar
Group Marsia Tillya na mtaalamu wa afya kutoka Shirika la Cardiostart International
la nchini Marekani Sarah King wakimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (ECHO) mwananchi aliyefika katika Hospitali hiyo wakati wa
kambi maalumu ya siku mbili ya kufanya vipimo vya moyo kwa wananchi wa Dar es
Salaam bila malipo.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika foleni ya kufanya vipimo vya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili ya kufanya vipimo vya moyo iliyokuwa ikifanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Cardiostart International la nchini Marekani katika Hospitali ya JKCI Dar Group iliyopo TAZARA jijini Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza Hospitali ya JKCI Dar Group kwa
kushirikiana na wataalamu wa afya kutoka Shirika la Cardiostart International
la nchini Marekani wamefanya kambi maalumu ya upimaji wa vipimo vya moyo kwa wananchi
wa mkoa wa Dar es Salaam.
Upimaji huo umefanyika kwa siku mbili ambapo wananchi
waliojitokeza wamepata fursa ya kupima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) pamoja na kipimo cha kuangalia mfumo
wa umeme wa moyo (Electrocardiography – ECG) bila malipo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii daktari wa Hospitali
ya JKCI Dar Group Marsia Tillya alisema uhitaji wa wananchi kupata huduma ya
vipimo vya moyo ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza
kupima kufanya vipimo hivyo.
Dkt. Marsia alisema watu waliojitokeza kufanya vipimo hivyo
wapo ambao walishawahi kupima na kukutwa na magonjwa ya moyo lakini kutokana
hali zao za uchumi hawakupata nafasi ya kupima tena hadi nafasi hiyo ilipojitokeza.
“Watu tuliowaona wapo ambao walishapima na kukutwa na shida
za moyo lakini pia wapo watu ambao hawakuwahi kupima moyo lakini kupitia kambi
hii wamepata fursa ya kupima na kufahamu hali zao”, alisema Dkt. Marsia
Kwa upande wake mtaalamu wa afya kutoka Shirika la
Cardiostart International la nchini Marekani Sarah King alisema wataalamu wa
afya wa Cardiostart mbali na kutoa huduma za upasuaji wa moyo pia walijipanga
kufanya vipimo vya moyo kwa wananchi bila malipo kuwapa nafasi ya kuchunguza
mioyo yao.
“Tumepanga kufanya vipimo vya moyo kwa watu wote
watakaojitokeza hivyo wasisite kufika katika Hospitali ya Dar Group kwani tupo
kwaajili yao”, alisema Sarah.
Sarah alisema sambamba na kuwafanyia wananchi vipimo vya moyo
pia wanapata muda wa kuzungumza na wananchi wanaofika katika kambi hiyo
kufahamu masuala muhimu ya afya zao na kuwajengea tabia za kupima afya zao mara
kwa mara kabla ya kuumwa.
Naye mwananchi aliyepatiwa huduma katika kambi hiyo Susan
Paul alisema amejitokeza kupima moyo wake kutokana na hapo awali alipata
maumivu makali ya moyo na kufika katika moja ya hospitali ambapo alipatiwa
huduma na kushauriwa kupima moyo wake.
Susan alisema baada ya kupata tangazo la upimaji wa vipimo
vya moyo katika Hospitali ya Dar Group aliona hiyo ndio fursa kwake kufika na
kupima moyo wake ili aweze kujua afya yake.
“Nashukuru sana kwa hii nafasi niliyoipata kuchunguza moyo
wangu mapema kwani kunanipa nafasi ya kujua kama lile tatizo nililokuwa nalo
awali linasababishwa na magonjwa ya moyo na kama sio nitajilinda ili nisije
kupata ugonjwa huu wa moyo”, alisema Susan.
Comments
Post a Comment