Wadau wakutana kujadili Mitaala ya mafunzo ya upasuaji wa moyo
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Godwin Sharau akichangia mada
wakati wa kiako cha kupitia mitaala ya program za mafunzo ya upasuaji wa moyo
na upasuaji wa tundu dogo zitakazofanywa na JKCI kwa kushirikiana na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Serena iliyopo
jijini Dar es Salaam
********************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wako mbioni kuanzisha kozi za upasuaji wa
moyo na upasuaji wa tundu dogo ili kuweza kukabiliana na changamoto ya upungufu
wa wataalamu wa upasuaji wa moyo nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao cha kujadili mitaala
itakayotumika kufundishia wataalamu watakaojiunga kupata mafunzo ya kibingwa ya
matibabu ya upasuaji wa moyo na upasuaji wa tundu dogo.
Dkt. Kisenge alisema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa
na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza mitambo mikubwa miwili katika
taasisi hiyo, uwekezaji ambao unahitaji kuongeza wataalamu wanaoweza kutoa
huduma za kibingwa za upasuaji wa tundu dogo.
“Programu ya mafunzo ya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu
dogo ni programu ya kwanza kufanyika Afrika mashariki, wataalamu wa afya
wasisite kujiunga kupata mafunzo haya muhimu yatakayowasaidia kwenda kuokoa
maisha ya wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema mafunzo hayo yatafanyika kwa kipindi cha
miaka mitatu kwa wataalamu wa afya wa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua na
kipindi cha miaka miwili kwa wataalamu wa afya wa upasuaji wa moyo kupitia
tundu dogo.
“Mshtuko wa ghafla wa moyo unasababishwa na mishipa ya damu
kuziba ambapo tunatumi njia ya tundu dogo kumtibu mgonjwa na matibabu haya
yanahitajika kufanyika ndani ya nusu saa hadi lisaa limoja mgonjwa awe amepata
huduma, kupitia mafunzo haya wataalamu wataenda kuongezeka na kusambaa nchi
nzima kuwasaidia wagonjwa na kupunguza vifo vya ghafla”, alisema Dkt. Kisenge
Aidha Dkt. Kisenge alisema katika ushirikiano huo waliouanzisha
na chuo kikuu cha Dar es Salaam pia watatoa mafunzo kwa wauguzi wanaowahudumia
wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na wagonjwa wa dharura
“Mafunzo kwa wauguzi wanaowahudumia wagonjwa wa dharura
tumeyaanzisha tangu mwaka 2021 ambayo pia yamewavutia watoa huduma wengi
wakiwemo kutoka nchini Rwanda na Zambia”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake Mkuu wa ndaki ya Afya na Sayansi za Afya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam tawi la Mbeya (UDSM) Prof. Projestine Muganyizi alisema
JKCI hapa nchini ndio hospitali pekee inayotoa huduma za matibabu ya moyo hivyo
UDSM ikaona ishirikiane nayo kutengeneza programu tatu za mafunzo kutatua
changamoto ya wataalamu bobezi wa tiba za upasuaji wa moyo na upasuaji wa tundu
dogo.
Prof. Muganyizi alisema kupitia programu hizo wamekusudia
kuongeza wataalamu wabobezi wa upasuaji wa moyo na wataalamu wa kuzibua mishipa
ya moyo nchini kwani uhitaji wa wataalamu hao bado ni mkubwa.
“Tumeamua kujikita katika kutoa mafunzo haya kwani mpango
mkakati wa chuo chetu, UDSM dhima 2061
inatuelekeza kutatua changamoto za kiafya na zile ambazo zinahitajika zaidi kwa
umma wa watanzania”, alisema Prof. Muganyizi
Prof. Muganyizi alisema kwa kushirikiana na JKCI inainda
kukipa chuo kikuu cha Dar es Salaam nafasi nyingine ya kutengeneza wataalamu
zaidi na kupeleka mafunzo na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo nyanda za
juu kusini.
Naye Msajili kutoka Baraza la Madaktari la Tanganyika (MCT)
Dkt. David Mzava alisema ushirikiano kati ya UDSM na JKCI unaenda kuongeza
juhudi ya Serikali katika kuhakikisha kuwa wataalamu wabobezi wanapatikana
wakutosha na kufikisha huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu na kwa urahisi.
“MCT imekuwa ikiangalia usalama wa wataalamu kuhakiksha
kwamba mgonjwa akihudumiwa ahudumiwe katika ubora unaohitajika, hivyo kupitia
programu za mafunzo zinakazofanywa na JKCI na UDSM zitaenda kuboresha huduma
zaidi”, alisema Dkt. Mzava
Dkt. Mzava alisema kuwa Baraza la madaktari la Tanganyika pia
limekuwa likishauri vyuo vinavyotoa mafunzo ya afya kushirikiana na hospitali kama
ambavyo UDSM na JKCI inaenda kufanya kuhakikisha kuwa ubora wa wahitimu
umehakikiwa na kulindwa.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na wadau wa sekta ya afya waungana
kupitia
Hatua ya kwanza ya kupitia mitaala ya kozi hizo imefanyika
mwishoni mwa wiki na kuhusisha wadau mbalimbali wa sekta ya afya ikiwemo Wizara
ya afya, Viongozi wa hospitali kubwa nchini na wajumbe kutoka Baraza la
Madaktari la Tanganyika (MCT).
Comments
Post a Comment