Kagera wafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Yona Gandye akizungumza na wataalamu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) pamoja na wa JKCI kabla ya kuanza kwa zoezi la siku tano la upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Kagera.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Dkt. Museleta Nyakiroto akizungumza na wataalamu wa afya wa hospitali hiyo pamoja na wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kabla ya kuanza kwa zoezi la siku tano la upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Kagera.
Baadhi wa wananchi wa Kagera waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) wakisubiri kwenda kufanyiwa vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography) na mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya (Electrocardiography) wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa wa Kagera.
Afisa Lishe waTaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo na Mtaalamu wa Tiba - Viungo Jenes Blasio wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) wakitoa elimu ya lishe bora na umuhimu wa kufanya mazoezi kwa wananchi waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo. Wataalamu wa JKCI wako mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
Kambi maalumu ya siku tano
ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo imeanza leo katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) iliyopo mkoani Kagera.
Kambi hiyo inafanywa na wataalamu wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH).
Katika kambi hiyo wananchi wanapata
huduma mbalimbali za upimaji wa moyo zikiwemo za vipimo vya kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo pia wanapata elimu na ushauri wa
lishe bora, matumizi sahihi ya dawa za moyo pamoja na matibabu ya kibingwa kwa
wale wanaokutwa na matatizo.
Akizungumzia leo na wafanyakazi wa
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na
mfumo wa mapigo ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Yona Gandye
alisema katika kambi hiyo wanatoa huduma za matibabu pamoja na kuwajengea uwezo
wataalamu wa BRRH ili waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo.
“Taasisi yetu imekuwa ikiwafuata
wananchi mahali walipo na kutoa huduma za tiba mkoba ya matibabu ya kibingwa ya
magonjwa ya moyo zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
Outreach Services kupitia huduma hii wananchi wengi wamepata matibabu ya moyo kwa
wakati”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande
wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Dkt. Museleta
Nyakiroto aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufika katika hospitali hiyo na
kushirikiana na wataalamu katika kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo.
“Ninaamini baada ya kumalizka kwa kambi hii wataalamu wetu watakuwa
wamepata utaalamu wa kutosha katika kutoa hudumoa za matibabu ya moyo”, Dkt.
Museleta Nyakiroto.
Dkt. Nyakiroto aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika kambi hiyo
ili waweze kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo pamoja na ushauri wa
lishe.
Comments
Post a Comment