Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa
watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu
kilichopo nchini Saudi Arabia wakifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu
ya moyo wa mtoto ambayo haijakaa katika mpangilio wake wakati wa kambi maalumu
ya upasuaji wa moyo inayofanyika JKCI.
**********************************************************************************************************************************************************************************************************************
Na Stela Gama – JKCI
Watoto 23 akiwemo wa umri wa siku tatu wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa
nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya
moyo kwa watoto inayofanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo maalumu ya upasuaji inafanywa na wataalamu
wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
wakishirikiana na wenzao wa kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu
kilichopo nchini Saudi Arabia.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi wa upasuaji
na daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi wa JKCI Dkt. Angela Muhozya
alisema kambi hiyo ni muendelezo wa ushirikiano mzuri uliopo na wenzao wa Saudi
Arabia katika kutibu watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo.
“Mpaka kufikia leo hii ni siku ya tano tangu kambi hii
imeanza na tumeweza kuwafanyia upasuaji
watoto wapatao 23 na tunatarajia kuwafanyia watoto 40 na kwa wale
waliofanyiwa upasuaji siku za mwanzo wanaendelea vizuri, wamesharuhusiwa kutoka
katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) wako wodini wanaendelea na matibabu”,
alisema Dkt. Angela.
Dkt. Angela alisema wameweza kumfanyia upasuaji wa
moyo mtoto mdogo mwenye umri wa siku tatu ambaye mishipa yake ya moyo haikuwa
katika mpangilio wake sahihi kama inavyotakiwa kuwa na kwa sasa anaendelea
vizuri.
“Tunawashukuru wenzetu wa Kituo cha Mfalme Salman cha
Misaada ya Kibinadamu kwa kujitoa kwao
kwani licha ya kutoa huduma za matibabu pia wametupatia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 ambavyo
vinatumika katika kufanya upasuaji huu wa moyo unaoendelea ”, alisema Dkt.
Angela.
Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo na mishipa ya
damu kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu Mohammad Shihata
alisema kambi hiyo imekuwa ikidhaminiwa na Mfalme Salman wa nchini Saudi Arabia
kuwawezesha watoto kupata matibabu na kubadilishana ujuzi na madaktari wa JKCI.
Dkt. Shihata alisema timu nzima ya watu 26 kutoka
nchini Saudi Arabia ambao ni waatalamu wa usingizi, waendesha mashine za moyo,
wauguzi na madaktari wameshiriki katika kambi hiyo ili kuhakikisha watoto wengi
wanafanyiwa upasuaji wa moyo.
“Hii ni siku yetu ya tano na ni mara ya yangu ya saba kuja
hapa nchini kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, siku zote tumekuwa tukipokea
ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari wa JKCI katika kufanikisha utoaji wa
huduma hii”, alisema Dkt. Shihata.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa
upasuaji wa moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema
kuwa imewasaidia kuokoa maisha ya watoto hao wenye matatizo ya moyo.
Zainabu Mussa kutoka mkoani Kigoma mzazi ambaye mtoto
wake amefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo alisema mtoto wake alikuwa anasumbuliwa
na ugonjwa ya moyo tangu alipomzaa na kumpeleka katika hospitali mbalimbali
bila ya mafanikio.
“Mwanangu alipofikisha umri wa miezi mitano hakuwa anaweza kukaa, anakosa
nguvu na kutoka jasho kwa wingi lakini hatukuweza kugundua mapema kama anashida
ya tundu kwenye moyo hadi pale wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
walivyofanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani Kigoma”,
alisema Zainabu.
“Namshukuru sana Mungu mara baada ya mtoto wangu kupatiwa
matibabu anaendelea vizuri, nawashukuru pia wataalamu wa JKCI kwanhuduma zao
nzuri na ningependa kuwashauri wazazi wasisite kuwapeleka watoto hospitali
endapo wataona watoto wao hawakui vizuri”, alisema Zainabu.
“Mwanangu aligundulika kuwa na shida ya moyo wakati
anatibiwa katika Hospitali ya mkoa Temeke baada ya kupewa rufaa ya kuja JKCI
aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo, namshukuru Mungu amefanyiwa upasuaji na
anaendelea vizuri”, alisema Zuhura Mkamba.
Comments
Post a Comment