Naibu Katibu Mkuu Ntonda avutiwa na utoaji wa huduma za matibabu ya moyo mkoani Mbeya
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Methusela Ntonda akizungumza na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda kuhusu kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo inafanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) katika mkutano wa 109 wa Wadau wa Elimu kwa Umma. Kushoto ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Patrick Mvungi.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akitoa elimu ya lishe bora kwa wananchi waliofika katika viwanja vya City Park Garden vilivyopo jijini Mbeya kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services. Huduma hizo zinazotolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
***************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Methusela Ntonda ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) kwa kutoa huduma za kibingwa za upimaji na matibabu ya moyo kwa wananchi.
Pongezi hizo amezitoa leo jijini Mbeya wakati akipewa taarifa
ya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo, huduma inayotolewa kwa washitiri wa mkutano wa 109 wa wadau wa Elimu kwa Umma
ulioandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na wananchi wa mkoa wa
Mbeya.
Ntonda alisema kutolewa kwa huduma za kipingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi
kutawasaidia kufahamu hali za mioyo yao na kuchukuwa hatua mapema ya kujilinda kwa
watakaokutwa wazima na wale wagonjwa kuanza matibabu mapema.
Akitoa taarifa ya upimaji huo Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na
Mawasiliano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anna Nkinda alisema kwa siku
moja ya jana (17/2/2025) waliona watu 139 kati ya hao watu wazima walikuwa 133
na watoto sita, waliohitaji kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupewa rufaa ya kwenda
kutibiwa JKCI walikuwa 12 kati ya hao watu wazima tisa na watoto watatu.
Anna alisema ili kusogeza karibu huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo kwa wananchi taasisi hiyo ilianzisha huduma ya uchunguzi na
matibabu kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ijulikana kwa jina la tiba mkoba
ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
“Huduma tunazozitoa ni za vipimo vya awali vya magonjwa ya
moyo vikiwemo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa
umeme wa moyo , tunatoa elimu ya lishe, matumizi sahihi ya dawa za moyo pia
tunawapatia wananchi vipeperushi vya lishe na kuufahamu ugonjwa wa shinikizo la
juu la damu”, alisema Anna.
Kambi hiyo ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanywa
na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, MZRH na
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) inafanyika katika viwanja vya City Park
Garden vilivyopo mkabala na uwanja wa mpira wa Sokoine jijini Mbeya.
Comments
Post a Comment