Wataalamu 50 wapatiwa mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi
Daktari
bingwa wa mifupa ambaye pia ni Mkufunzi kutoka Kituo cha mafunzo cha tiba na
huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) Sylvester Faya
akimuonesha baadhi ya vifaa vinavyotomika kutoa mafunzo kwa wataalamu wanaotoa huduma
za dharura na kwa wagonjwa mahututi Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo
yanayofanyika katika ukumbi wa JKCI leo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akizungumza na washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya dharura na kwa wagonjwa mahututi wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo leo jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yameandaliwa na Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA).
Daktari
bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi kutoka nchini Australia John Botha
akielezea umuhimu wa kupata mafunzo ya kutoa huduma za dharura mara kwa mara
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo uliofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) leo jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yameandaliwa na Kituo cha
mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA).
Daktari
bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi kutoka nchini Australia Mariepaz
Chang Hazell akichangia mada wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya dharura na kwa
wagonjwa mahututi yaliyoandaliwa na Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za
dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) na kufunguliwa leo katika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya siku mbili ya dharura na kwa wagonjwa mahututi wakisikiliza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) na kufunguliwa leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Na: JKCI
**************************************************************************************************************************
Wataalamu 50 wanaotoa
huduma za matibabu ya dharura, na matibabu kwa wagonjwa mahututi kutoka
hospitali mbalimbali nchini wameshiriki katika mafunzo ya kuongeza ujuzi katika
fani ya huduma za dharura na mahututi.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema mafunzo hayo ya siku mbili
yameandaliwa na Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency
Medicine Services Academy – EMSA) na kufanyika JKCI.
Dkt. Waane alisema
katika mafunzo hayo pia wamepata wataalamu wanaotoa huduma za dharura kutoka
nchi za New Zealand, Australia ambao wataongeza ujuzi zaidi kwa wataalamu wa
hapa nchini.
“Serikali yetu imejenga
vyumba vya wagonjwa mahututi na kutoa vifaa tiba kwaajili ya matibabu hayo
katika hospitali mbalimbali nchini, hivyo kupitia mafunzo haya tutaweza kuwajengea
uwezo wataalamu wa afya na kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa wanaotutegemea”,
alisema Dkt. Waane
Kwa upande wake Daktari
bingwa wa mifupa ambaye pia ni Mkufunzi kutoka Kituo cha mafunzo cha tiba na
huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) Sylvester Faya
alisema mwitikio wa wataalamu kushiriki katika mafunzo hayo hapo awali ulikuwa
mdogo tofauti na ambavyo sasa watu wanashiriki kwa wingi.
Dkt. Faya alisema
kupitia mafunzo hayo wanategemea huduma za matibabu ya dharura na kwa wagonjwa
mahututi yaongezeke ili wagonjwa waweze kutibiwa kwa ujuzi wa hali ya juu.
“Kupitia mafunzo haya
tumeanza kupokea wataalamu kutoka nje ya nchi kushiriki mafunzo kwani hadi sasa
tumeshatoa mafunzo kwa wataalamu kutoka Sudan, na sasa tuna maombi ya ushiriki
kutoka Kenya, na Zambia”, alisema Dkt. Faya.
Naye mshiriki wa
mafunzo hayo kutoka Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Mwanahawa Hamidu alisema hii
ni mara yake ya pili kushiriki mafunzo hayo yanayomuwezesha kutoa huduma bora
na kufanya maamuzi kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.
Dkt. Mwanahawa alisema
mafunzo aliyoyapata mwanzo yamekuwa chachu kwake kumfanya ashiriki kwa mara ya
pili ili aweze kujifunza zaidi na kwenda kurahisisha matibabu huku akiokoa
maisha ya wagonjwa anaowahudumia.
“Fursa hizi zinapotokea
kwetu madaktari zinatusaidia kuongeza ujuzi, kwani kama una vitu viwili ndani
yako hapa utatoka na vya ziada vitatu au vinne hivyo kuboresha huduma zaidi”,
alisema Dkt. Mwanahawa
Wataalamu hao wametoka
katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), Shree Hindu Mandal, Hospitali ya
Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila (MNH), Bugando Medical Center, Taasisi ya
Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya
Mananyamala, wataalamu kutoka Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha Aga Khan, na
Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Comments
Post a Comment