Wananchi Mbeya waishukuru Serikali kuwafikishia huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Loveness Mfanga akichukua taarifa za mwananchi aliyefika katika viwanja vya City Park Garden vilivyopo jijini Mbeya kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari akimuhudumia mwananchi aliyefika katika viwanja vya City Park Garden vilivyopo jijini Mbeya kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services. Huduma hizo zinazotolewa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wananchi wa mkoa wa Mbeya wameipongeza Serikali kwa kufikisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani humo zijulikanazo kwa jina la tiba mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
Shukrani hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na wananchi hao
waliofika leo katika viwanja vya City Park Garden kwa ajili ya kupata huduma hizo
zinazotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya
Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Moses Mwambungu kutoka Kyela alisema miaka mitatu iliyopita
aliandikiwa kwenda katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufanya vipimo
vya moyo lakini kutokana na uwezo wake kiuchumi kuwa mdogo alishindwa kusafiri
kwenda Dar es Salaam, baada ya kusikia huduma hizo zitakuwepo mkoani Mbeya
aliona atumie nafasi hiyo kupima.
“Nimefika jana kutoa Kyela nimelala katika viwanja hivi
kwaajili ya kusubiri kupata huduma, nashukuru nimefanya vipimo vyote vya moyo na
nimekutwa sina shida kwani miaka ya nyuma niliwahi kupima mahali nikaambiwa
nina tundu kwenye moyo”.
“Baada ya vipimo nimekutwa na shida ya presha iko juu
nimeandikiwa dawa za kutumia na kuelekezwa kufanya mazoezi na kula chakula bora
ili presha yangu ikae sawa”, alisema Mwambungu.
Mama Ulimbaga Mwasaga mkazi wa Mwanjela ambaye alihisi mjukuu
wake anaweza kuwa na shida ya moyo kwani anakohoa sana hasa kipindi cha baridi
na akaona ampeleke kwa wataalamu wa moyo ili afanyiwe vipimo.
“Baada ya kufanya vipimo wamekuta mjukuu wangu yuko sawa na
hana shida yoyote ya moyo daktari amesema anatatizo la aleji amemuandikia dawa
za kutumia.Ninatoa wito kwa wananchi wenzangu waje kupima afya zao kwani huduma
zimewafikia mlangoni waje kupima”, alisema Mama Ulimbaga.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto
wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Stella Mongella alisema wataalamu wa
taasisi hiyo wako katika mkoa huo kwaajili ya kutoa huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo.
“Tunatoa huduma za kibingwa kwa watoto na watu wazima huduma
tunazozitoa ni tunafanya vipimo vya kuangalia sukari kwenye damu, uwiano baina
ya urefu na uzito, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi, mfumo wa
umeme wa moyo na elimu ya lishe bora”, alisema Dkt. Stella.
Dkt. Stella alisema huduma hiyo inatolewa bila malipo yoyote hivyo
basi aliwaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kupima afya za mioyo yao na kupata
ushauri wa kitaalamu wa matumizi sahihi ya dawa za moyo na elimu ya lishe bora.
Comments
Post a Comment