Wakazi wa Mbeya wanufaika na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo

Watafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakichukua taarifa
za wananchi waliofika katika viwanja vya City Park Garden vilivyopo jijini
Mbeya kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa
na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) na Shirika
la Utangazaji Tanzania (TBC).
Wakazi wa mkoa wa Mbeya wakisubiri kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika katika viwanja vya City Park Garden. Huduma hiyo inatolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Kanda
Mbeya (MZRH) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
*********************************************************************************************************************************************************************************************
WAGONJWA 360 wamehudumiwa katika siku tatu za kwanza za Kambi ya siku tano ya uchunguzi bure wa magonjwa ya Moyo inayoendelea mkoani Mbeya chini ya madaktari bingwa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikishirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH).
Hayo yamebainishwa leo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto kutoka JKCI, Dkt. Stella Mongella alipozungumzia mwenendo wa utoaji wa huduma ya kibingwa bobezi ya magonjwa ya moyo ijulikanayo kama Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge.
Kwa mujibu wa tangu kuanza kwa kambi hiyo Februari 17 mwaka huu kwa siku tatu za awali wagonjwa wapatao 360 wamehudumiwa kati yao wakiwemo watu wazima 340 na watoto walikuwa 20 na miongoni mwa wagonjwa hao 34 walihitaji rufaa.
Alizitaja huduma zilizotolewa kuwa ni pamoja na mteja kumuona daktari,kupimwa uzito na urefu,sukari na shinikizo la damu ambapo kwa walioonekana kuwa na viashiria vya shida ya moyo walifanyiwa pia vipimo vya ziada vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi na mfumo wa umeme wa moyo.
“Maradhi mengine ya moyo ambayo tumeyakuta yanawakabili wananchi wa hapa ni Moyo kupanuka, kuwepo na shida kwenye mishipa ya damu iliyopo kwenye moyo na shida za kwenye milango ya moyo ijulikanayo kama valvu.”, alisema Dkt.Stella.
“Kwa wale wenye shinikizo la juu la damu inaonekana pia wengi wanakuwa na shida ya kisukari. Na kisukari inafahamika ni kati ya visababishi vikubwa vya kuwa na shinikizo la juu la damu.”, aliongeza.
Alifafanua kuwa malengo ya kambi hiyo ni kuleta huduma ya kibingwa bobezi kwa wananchi,kukuza ushirikiano baina ya JKCI na watoa huduma wengine ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, kuwaona wagonjwa walio na uhitaji wa kupata huduma mapema na watafiti kukusanya taarifa juu ya changamoto zinazohusiana na magonjwa ya moyo.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Dkt. Godlove Mbwanji,Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dkt. Gloria Mbwile aliipongeza JKCI kwa kuwashirikisha akisema kambi hiyo pamoja na kutoa huduma bure kwa wahitaji pia inawaongezea utaalamu wataalamu wa hospitali hiyo.
Kwa upande wao wanufaika wa kambi hiyo Shukrani Mginah,Rahma Omary na Noel Alfred walishukuru Taasisi hiyo kwa kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kufuata huduma hizo.
Comments
Post a Comment