JKCI yatoa mafunzo ya awali ya kuokoa maisha kwa waongoza watalii Zanzibar
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor
Ahmed Mazrui akizungumza na wataalamu wa afya jana katika ukumbi wa mikutano wa
Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa
magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025 utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 mwezi Aprili
mjini Zanzibar. Mkutano huo unasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI).
Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Dkt. Amoor Mohamed akielezea changamoto ya magonjwa ya moyo ilivyo Zanzibar
wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025
utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 Aprili jana katika ukumbi wa mikutano wa
Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) mjini Zanzibar.
Baadhi ya viongozi kutoka mashirika mbalimbali Zanzibara
wakifuatilia wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo
(CardioTan) 2025 utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 Aprili jana katika ukumbi wa
mikutano wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) mjini Zanzibar.
Mratibu wa mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na
mahututi kutoka Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency
Medicine Services Academy – EMSA) Ebony Ford akiwafundisha waongoza watalii
Zanzibar mafunzo ya awali ya kuokoa maisha baada ya uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025
utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 Aprili jana katika ukumbi wa mikutano wa
Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) lililopo mjini Zanzibar.
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Shamira Rwegoshora akiwafundisha mafunzo ya awali ya kuokoa maisha waongoza watalii Zanzibar baada ya
uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025 utakaofanyika
tarehe 10 hadi 12 Aprili jana katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Bima la
Zanzibar (ZIC) lililopo mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Nassor
Ahmed Mazrui akiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane na viongozi kutoka
mashirika mbalimbali Zanzibar jana katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Bima
la Zanzibar (ZIC) wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo
(CardioTan) 2025 utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 mwezi Aprili mjini Zanzibar.
Mkutano huo unasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Na: JKCI
******************************************************************************************************
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kushirikiana na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika masuala ya utafiti, kinga na
matibabu ya magonjwa ya moyo huku ikidhamiria kuleta mabadiliko makubwa katika
sekta ya afya na utalii nchini.
Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui wakati wa uzinduzi wa mkutano wa tatu wa
magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025 utakaofanyika tarehe 10 hadi 12 mwezi Aprili
mjini Zanzibar ulioenda sambamba na mafunzo ya siku mbili ya awali ya kuokoa maisha kwa watu wanaoongoza watalii Zanzibar.
Mhe. Mazrui alisema
JKCI imekuwa na mchango mkubwa katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mdau wa
karibu kushirikiana nao katika kutoa huduma za kibingwa bobezi za magonjwa ya
moyo kwa wananchi wa Zanzibar.
“Wagonjwa wengi wanaosumbuliwa na maradhi ya moyo
yaliyoshindikana kutibiwa hapa Zanzibar wamekuwa wakichukuliwa na kutibiwa
katika Taasisi hii. Kwa mwaka 2024 wagonjwa 624 kutoka Zanzibar wametibiwa JKCI”,
alisema Mhe. Mazrui
Mhe. Mazrui alisema sambamba na uzinduzi wa mkutano huo JKCI
imefanya mafunzo ya siku mbili kwa waongoza watilii Zanzibar ya kutoa huduma
ya awali ya kuokoa maisha wakiwa na lengo
la kuwajengewa uwezo wakuweza kutoa msaada sahihi na wa haraka pale huduma ya
kwanza na ya kuokoa maisha itakapohitajika.
“Leo tumeanza na nyie waongoza watalii, hii ni fursa adhimu mkiweza
kufahamu namna ya kutoa huduma hii itasaidia kuimarisha na kukuza uchumi wa
nchi kwa kuweza kuingiza idadi kubwa ya watalii nchini”, alisema Mhe. Mazrui
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema JKCI imefanya uzinduzi huo ikiwa
ni ishara ya kuelekea mkutano wa tatu wa magonjwa ya moyo (CardioTan) 2025.
Dkt. Waane alisema Mkutano wa CardoTan 2024 ulikuwa na
mafanikio makubwa na kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu baina ya wataalamu
mbalimbali wa sekta ya afya nchini na kuhusisha wataalamu wa afya kutoka nchi
40 ambao walipata elimu ya magonjwa ya moyo na kujenga mashirikiano baina ya
nchi hizo.
“Mkutano wa CardioTan 2024 wataalamu wa afya walipata fursa
ya kuweza kubaini viashiria vya magonjwa ya moyo, uchunguzi na matibabu yake
pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo katika magonjwa haya”, alisema Dkt.
Waane
Dkt. Waane alisema mafunzo ya awali ya kuokoa maisha yanaenda sambamba na uzinduzi wa mkutano huu ambayo ni muendelezo wa
yale yaliyokuwa wamekubalika na kutekeleza maazimio ya mkutano wa mwaka 2024
kuwasaidia wananchi na watalii wanaotembelea visiwa vya Zanzibar.
“Tunaamini kuwa mafunzo haya yataleta tija kwenye mnyororo wa
thamani ya utalii pamoja na utalii tiba kwa kusaidia kuongeza utambuzi na kutoa
msaada wa haraka pale inapotokea changamoto ya afya katika jamii ama kwa
watalii wetu”,
“Ujuzi na uwezo wa kuokoa maisha wakati wa dharura huongeza
uelewa wa afya na usalama katika jami hivyo itasaidia sekta ya utalii kwa kuhakikisha kuwa
kuna watu wanaweza kutoa msaada wa haraka pale inapohitajika na kuitangaza
Zanzibar kama eneo salama kwa watalii hivyo kuongeza imani kwa wageni wetu”,
alisema Dkt. Waane
Naye Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Dkt. Amoor Mohamed alisema mafunzo ya awali ya kuokoa maisha yanahitajika kwa kiasi kikubwa Zanzibar kwani tafiti zinaonesha kuwa
sababu inayochangia kuwa na vifo vingi vya watoto wachanga, akina mama na
wagonjwa wa ajili vinatokana na upungufu wa taaluma ya kuokoa maisha.
Dkt. Mohamed alisema suala la maisha halina mbadala hivyo
kuwataka wataalamu wa afya na watu wenye ujuzi na mafunzo ya kutoa huduma ya
kwanza wanatumia taaluma yao kurudisha maisha ya mtu ambaye moyo wake umesita.
“Tujitoe kuhakikisha tunaokoa maisha ya binadamu wenzetu.
Uokozi wa maisha si lazima ufanyike Hospitali unaweza kufanyika kokote, hivyo kila
mtu ahakikishe kuwa ana uwezo wakuokoa maisha ya mwenzie pale moyo unaposimama
ghafla”, alisema Dkt. Mohamed
Comments
Post a Comment