Wataalamu wa Tehama wapimwa moyo Arusha
Fundi Sanifu wa Moyo (Cardiovascular technologist) wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Sven Kamugisha akimuelezea huduma zinazotolewa na
taasisi hiyo mshiriki wa mkutano wa tano wa mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)
alipofika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za uchunguzi
wa magonjwa ya moyo katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
jijini Arusha.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mshiriki wa mkutano wa tano wa
mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) unaofanyika katika kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura kutoka Hospitali ya
Mount Meru Nullugendo Mushi akimsikiliza afisa Tehama aliyeshiriki katika
mkutano wa tano wa mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) alipofika katika banda la
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kufanya vipimo vya moyo leo
katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) jijini Arusha.
Na: JKCI
******************************************************************************************************
Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameweka kambi maalumu ya siku tatu ya uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wataalamu wa Tehama.
Kambi hiyo maalumu ijulikanayo kwa jila la Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan tiba Mkoba inafanyika wakati wa mkutano wa tano wa mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA) katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha
(AICC) jijini Arusha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii leo Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Salehe Mwinchete
alisema mwitikio umekuwa mkubwa kwani maafisa tehama wametuma fursa hiyo
kujitokeza kupima afya zao.
Dkt. Salehe alisema sambamba na kutoa huduma za uchunguzi wa
magonjwa ya moyo katika kambi hiyo pia wanatoa elimu ya magonjwa hayo na namna
ya kukabiliana nayo.
“JKCI imeamua kuwafikia wataalamu wa Tehama kama ambavyo
imekuwa ikiwafikia wataalamu wa kada nyingine nchini lengo likiwa kujenga taifa
lenye afya bora”,
“Tumekuja kuwapa huduma bobezi za uchunguzi wa magonjwa ya
moyo kwa kutumia mashine zetu za kisasa zinazoweza kutambua matatizo mbalimbali
ya moyo msisite kufika na kupata huduma”, alisema Dkt. Salehe
Kwa upande wake mshiriki wa mkutano huo Daud Simbeye
aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufikisha huduma hizo kwa wataalamu wa
Tehama kwani watu wengi hawana tabia za kufanya uchunguzi wa afya hadi pale
wanapoumwa.
Daud alisema amekuwa akifanya uchunguzi wa afya yake mara kwa
mara kila anapopata fursa ya kuchunguza afya hivyo akaona ni muhimu pia kutumia
fursa hii ya kupima moyo wake.
“Mimi nimekuwa muumini mzuri sana wa kuchunguza afya yangu
mara kwa mara, kila ninapokuta kambi za uchunguzi wa afya sisiti kupima kwani
naamini kwa kufanya hivyo ninajijua zaidi na naweza kufanya maamuzi mazuri
yanayoendana na afya yangu”, alisema Daud
Naye Sophia Mgaya mshiriki wa mkutano huo aliwapongeza
wataalamu wanaotoa huduma kwa kuwapa elimu ya namna ya kujikinga na magonjwa ya
moyo na kuwahamasisha kuwa na mtindo bora wa maisha ili waweze kuepukana na
magonjwa yasiyoambukiza.
“Nimefurahi sana kufika katika Kliniki hii, nimepata huduma
kwa muda wa dakika ishirikini nimefanyiwa vipimo na kumuona daktari lakini pia
nimepata elimu ya lishe na namna ya kujilinda na magonjwa haya”, alisema Sophia
Comments
Post a Comment