TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI MAFANIKIO YALIYOPATIKANA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA MINNE YA UONGOZI WA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
*************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ni Hospitali maalum na Chuo Kikuu cha mafunzo ya utaalamu wa matibabu ya moyo inayomilikiwa na Serikali inayotoa mafunzo na huduma za utafiti wa moyo. Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeona jumla ya wagonjwa 745,837 kati ya hao watu wazima walikuwa 674,653 na watoto 71,184 wagonjwa waliolazwa walikuwa 30,645 watu wazima wakiwa 25,273 na watoto 5,372.
Wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Upanga walikuwa 513,484 kati ya hao watu wazima 470,119 na watoto 43,365 wagonjwa waliolazwa walikuwa 17,668 watu wazima wakiwa 14,580 na watoto 3,088.
Katika hospitali yetu ya Dar
Group iliyopo eneo la TAZARA tumetibu wagonjwa 278,839 kati yao
watu wazima walikuwa 238,570 na Watoto 40,269. Wagonjwa waliolazwa walikuwa
12,977 watu wazima 10,693 na watoto 2,284. Huduma tulizozitoa ni za
matibabu ya moyo, kinywa na meno, huduma za dharura, kliniki ya wanawake na
wajawazito, kliniki ya watoto, macho, pua, masikio na koo, kliniki ya ngozi,
vibofu vya mkojo, upasuaji mkubwa na mdogo, magonjwa ya tumbo na ini, figo na
matibabu mengine ya magonjwa yanayoambukiza kama malaria.
Huduma za tiba mkoba
zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services zimetolewa
katika mikoa 20 na maeneo ya kazi 14 kwa watu 21,324 watu wazima wakiwa 20,112
na watoto 1,212 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo. Kati
ya hao 8,873 watu wazima wakiwa 8,380 na watoto 493 walikutwa
na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 3,249 watu
wazima 2,765 na watoto 484 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya
kibingwa na kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
Wataaamu wetu walivuka mipaka ya nchi na kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo katika nchi za Malawi, Zambia na Jamhuri ya Watu wa Comoro wakiwa katika nchi hizo walitibu wagonjwa 1,189 watu wazima walikuwa 851 na watoto 338. Wagonjwa 262 walipewa rufaa ya kuja kutibiwa JKCI.
Wagonjwa waliotibiwa kutoka nje ya nchi walikuwa 689. Wagonjwa hao walitoka katika nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Watu wa Comoro , Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Congo, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa na Uingereza.
Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery –CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 2,784 kati ya hao watu wazima walikuwa 1,880 na watoto 904.
Upasuaji mpya wa moyo wa kufungua kifua uliofanyika ni wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu uliotanuka kwenye kifua na tumbo, kurekebisha valvu za moyo kwa watu wazima, kurekebisha mshipa uliotanuka kwenye bega, kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unafanya kazi bila ya kuusimamisha, kukarabati mlango wa moyo wa mshipa mkubwa wa damu iendayo kwenye mapafu kwa kutumia chumba cha moyo cha juu kulia, kutoa dawa ya kuzuia maumivu sehemu ya uti wa mgongo wakati wa upasuaji mkubwa wa moyo.
Kupitia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambao ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalum wagonjwa 8,789 walipata huduma ya matibabu kati yao watu wazima walikuwa 7,997 na watoto 792. Wagonjwa hawa walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo. Wagonjwa 469 walitibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo kwa kutumia mtambo wa kawaida na 109 walitibiwa kwa kutumia mtambo wa Carto 3.
Matibabu mapya yaliyofanyika katika mtambo wa Cathlab ni upasuaji wa moyo kwa njia ya tundu dogo wa kurekebisha mishipa ya damu iliyotanuka na kupasuka sehemu ya kifua na tumbo. Upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI), kutanua valvu za moyo kwa muda, uchunguzi na kufanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu (Peripheral Interventions) ambayo haipitishi damu vizuri na kuzibua mishipa ya damu ya shingoni.
Ili wananchi wengi zaidi wafikiwe na huduma zetu tumefungua kliniki mbili za matibabu ya moyo zilizopo Kawe katika jengo la Mkapa Health Plaza na nyingine Oysterbay katika jengo la Oyster Plaza. Huduma tunazozitoa ni za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima, kliniki za mishipa ya damu, huduma za maabara (ISO 15189:201), Fiziotherapia (Mazoezi tiba), huduma ya matibabu majumbani, elimu ya afya, lishe bora na mafunzo kwa jamii, huduma ya matibabu ya magonjwa ya ndani, duka la dawa, tiba mtandao, huduma ya gari la wagonjwa na huduma ya upimaji wa afya kwa vikundi mbalimbali.
Katika kuboresha
huduma za afya mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni uliogharimu shilingi
milioni 526,604,116 umefungwa katika Hospitali ya Dar Group pia
mtambo mwingine wa kuzalisha hewa ya oksigeni wenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 umefungwa
katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Mitambo hii inatumika kusambaza
hewa ya oksijeni kwa wagonjwa wenye uhitaji
na kupunguza gharama za kununua
mitungi ya oksijeni kama ilivyokuwa awali.
Taasisi yetu imesaini mikataba ya miaka
mitatu ya makubaliano na Hospitali za Taifa za nchini Rwanda na Zambia ya
kutibu wagonjwa wa moyo pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa
hospitali hizo wa jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo.
Pia tumesaini mikataba na Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam na Chuo cha Madaktari wa Upasuaji Afrika Mashariki, Kati na kusini mwa
Afrika (COSECSA) katika kutoa mafunzo bobezi ya matibabu ya moyo kwa
wataalamu wa afya, Chuo Kikuu cha Jagiellonian cha nchini Poland na Chuo Kikuu
cha New York kilichopo nchini Marekani kwa ajili ya kufanya utafiti, elimu na
utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa moyo. Tumesaini mkataba na Taasisi ya
Afya Ifakara (IHI) kwa ajili ya kufanya utafiti wa magonjwa ya moyo.
Kupitia kozi ya miezi sita ya mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa mahututi na wa dharura inayotolewa kwa wauguzi kati ya wanafunzi 85 waliomaliza wanafunzi watatu walitoka katika Hospitali za King Faisal iliyopo nchini Rwanda na 10 walitoka Hospitali ya Taifa ya Moyo ya nchini Zambia.
Shilingi bilioni 2.16
zilitolewa na Serikali kwaajili ya ukarabati wa vyumba vya watoto mahututi na
chumba cha wagonjwa mahututi cha watu wazima, ukarabati na utanuzi wa ICU ya
watoto ambayo hapo awali ilikuwa na vitanda nane na hivi sasa inavitanda 16 na
ICU ya wakubwa ambayo imetanuliwa na kuwa na vitanda kumi kutoka nane ambapo
shilingi 503,450,051 zilitumika katika ukarabati huo. Shilingi 1,465,683,469
zilitumika kununua vifaa tiba, shilingi 170,000,000 zilitumika kwa ajili ya
tiba mtandao (Telemedicine) na shilingi 28,340,000 zilitumika kugharamia
mafunzo ya wataalamu wa fani ya radiolojia na huduma za wagonjwa mahututi.
Serikali kupitia Sekretarieti
ya Ajira katika Utumishi wa Umma imeajiri wafanyakazi
wapya 186 wa kada
mbalimbali, wafanyakazi 366 wamepandishwa
vyeo katika madaraja mbalimbali. Taasisi iliwaongezea ujuzi wa kazi wafanyakazi
kwa kuwapeleka kozi na muda mfupi watumishi 184, waliomaliza masomo ya kozi za
muda mrefu ni 45 na waliopo masomoni ni 51.
Kukamilika kwa ujenzi wa
jengo la ghorofa nne la utawala na vipimo ambalo limegharimu kiasi cha shilingi
bilioni 3.6 kumepunguza changamoto ya ofisi za wafanyakazi pamoja na wagonjwa
kupata eneo kubwa la kufanyiwa vipimo mbalimbali vya moyo.
Utoaji wa huduma bora na za
kisasa za matibabu ya moyo kumezifanya nchi mbalimbali kuja katika Taasisi yetu
kwaajili ya kujifunza, kuomba ushirikiano katika matibabu ya moyo na kuona
namna ambavyo tutawasaidia ili nao wafikie hatua tuliyofikia sisi katika utoaji
wa huduma za matibabu ya moyo. Baadhi ya nchi hizo ni Malawi, Somalia, Burundi, Zambia, Jamhuri
ya Watu wa Comoro , Burkina Faso, Nigeria,
Msumbiji, Gambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sierra Leone.
Ninaishukuru sana Serikali ya
awamu wa sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kutuunga mkono kazi tunazozifanya na kuhakikisha tunapata mahitaji yote muhimu
ikiwemo vifaa tiba vya kisasa ambavyo vinatuwezesha kutoa huduma bora kwa
wagonjwa wetu. Nasi tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora na kwa wakati kwa
wagonjwa tunaowahudumia.
“Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Letu”.
Imetolewa na:
Dkt. Peter Kisenge
Mkurugenzi Mtendaji
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
Comments
Post a Comment