Singida wafurahia huduma za matibabu ya moyo
Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Hospitali ya Dar Group Devotha Bertram akimpima kipimo cha kuangalia jinsi
mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography – ECG) mkazi wa
Singida aliyefika katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya
Mahali Pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Mandewa mkoani
Singida.
Na: Jeremiah Ombelo
*************************************************************************************************************
Wananchi wa Mkoa wa Singida wamepongeza huduma zinazotolewa
na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki
ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi mwaka 2025.
Maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya maonesho
Mandewa mkoani Singida ambapo taasisi hiyo inatoa huduma za uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi bila gharama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameelezea
furaha yao kutokana na huduma walizopata kutoka kwa wataalamu wa afya
waliobobea na wenye uzoefu kuhusu Magonjwa ya Moyo.
Mwahija Doe, mmoja wa wananchi wa Singida waliotembelea banda
la Taasisi hiyo, alisema huduma alizopata za kuchunguza moyo wake zimemfurahisha
na kuwasihi wananchi wengine kutembelea banda hilo kupata fursa ya kupima mioyo
yao.
“Nimepima shinikizo la damu (BP), sukari kwenye damu,
nimefanya kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography –
ECHO) na nimeonana na daktari bila gharama zozote, pia nimepokelewa vizuri
huduma zao ni nzuri sana”, Alisema Doe.
Kwa upande wake, Seif Mwendo ameipongeza Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) kwa namna ambavyo inatoa huduma kwa wananchi wa Singida
kwa weledi na kwa upendo.
“Kwa leo ukiniuliza upande wangu, Taasisi hii wamekuwa namba
moja, hii ni kutokana na jinsi walivyonipokea, kuniuliza maswali kuhusu afya
yangu, kunipima kwa utaratibu na kunielewesha vizuri ”, Alisema Mwendo.
Wananchi hao wameonesha kuridhika na kiwango cha huduma
walizopatiwa kutoka kwa wataalamu wa afya wa JKCI ambao walikuwa na usikivu na
kutoa elimu kwa kina kuhakikisha kila mwananchi anaondoka na uelewa sahihi wa
hali ya afya yake na kuifanya jamii kuhamasika zaidi katika kufanya uchunguzi
wa afya ya moyo.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) itaendelea kutoa huduma
za vipimo na ushauri wa afya katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na
Afya Mahali pa Kazi hadi tarehe 30 Aprili mwaka huu.
Katika maonesho hayo, taasisi hiyo inatoa huduma mbalimbali
za uchunguzi na matibabu ya moyo ikiwa ni pamoja na vipimo vya moyo, ushauri wa
afya, pamoja na elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya Moyo.
Huduma hizo zimeonekana kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wengi waliopata fursa ya kupima afya zao na kupata ushauri wa kitaalamu bila gharama yoyote.
Comments
Post a Comment