Waingizaji na wasambazaji wa vifaa tiba wakutana mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wataalamu kutoka kampuni ya uingizaji na
usambazaji wa vifaa tiba Kas Medics Limited alipotembelea banda la maonesho la
kampuni hiyo wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo
unaofanyika Zanzibar.
Washiriki wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wakipata elimu kuhusu matumizi ya vifaa tiba katika banda la maonesho la Bohari Kuu ya Dawa wakati wa mkutano huo unaondelea Zanzibar.
Mwakilishi kutoka Kampuni ya Snibe Diagnostic Flora M. Kawa
akiwaelezea wataalamu wa famasia kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
huduma zinazotolewa na kampuni hiyo wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa
magonjwa ya moyo unaofanyika Zanzibar.
Washiriki wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo
wakipata elimu katika banda la maonesho la kampuni ya Bariki Pharmacy wakati wa
mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo unaofanyika Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na maafisa kutoka Benki ya CRDB
baada ya kutembelea banda la Benki hiyo wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa
wa magonjwa ya moyo unaofanyika Zanzibar.
Picha na: JKCI
*******************************************************************************************************
Waingizaji na Wasambazaji wa vifaa tiba na dawa za binadamu kutoka
kampuni mbalimbali duniani wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
kwa kuwakutanisha pamoja kuonesha bidhaa zao wakati wa mkutano wa tatu wa
kimataifa wa magonjwa ya moyo.
Mkutano huo unaofanyika kwa siku tatu katika hoteli ya Sea
Clif & Spa iliyopo Zanzibar umewakutanisha wataalamu wa magonjwa ya moyo na
wasambazaji wa vifaa tiba na dawa kutoka nchi 25 duniani.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hii kwa nyakati tofauti wataalamu
hao wa vifaa tiba walisema maonesho hayo yamewakutanisha na watumiaji wa vifaa
wanavyozalisha jambo ambalo limewasaidia kuzifahamu zaidi vifaa hivyo.
Meneja mauzo kutoka kampuni ya Novomed inayosambaza vifaa
tiba nchini Michael Mchagi alisema kampuni hiyo imeshiriki katika mkutano huo
kama mdau wa afya upande wa vifaa tiba na kuunga mkono jitihada za Serikali
katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Michael alisema kampuni hiyo imefaidika kupitia mkutano huo
kwani imepata fursa ya kuonesha vifaa tiba kwa watoa huduma za afya pamoja na
kukutana na wataalamu mbalimbali katika kada ya afya ambao kwapamoja wameweza
kubadilishana ujuzi.
“Tumepata mapokeo mazuri kwa wataalamu waliotembelea banda
letu, tumepata ahadi za kushirikiana kwa pamoja lengo likiwa kurahisisha
upatikanaji wa vifaa tiba na kuboresha huduma za matibabu ya moyo nchini”,
alisema Michael
Kwa upande wake Meneja mauzo kutoka kampuni ya Neusoft
Medical System iliyopo nchini China Dkt. Kev Sheng alisema Kampuni hiyo
imeshiriki katika mkutano huo upande wa maonesho ya bidhaa kama sehemu ya kuionesha
dunia mashine za kisasa za Cathlab inazosambaza.
Dkt. Kev alisema ushiriki wao katika mkutano huo utawasaidia
kutengeneza mtandao mkubwa na wataalamu wa afya kutoka sehemu mbalimbali
duniani na kujenga mahusiano mazuri katika kuwasaidia wagonjwa wa moyo.
“Vifaa tunavyosambaza ni vya kisasa na kama vitawekezwa
katika hospitali zetu vitasaidia kuboresha huduma na kuokoa maisha ya wagonjwa
wa moyo”, alisema Dkt. Kev
Naye Meneja kutoka Hospitali ya Andalusia Health Group
iliyopo nchini Misri Dkt. Islam Samir alisema Hospitali hiyo imekuwa na
ushirikiano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika masuala mbalimbali
ikiwemo kubadilishana ujuzi na kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo.
Dkt. Islam alisema Hospitali ya Andalusia ipo tayari
kuwasaidia wagonjwa wa moyo waliopo Tanzania kupitia kambi mbalimbali za
matibabu ya moyo pamoja na kubadilishana ujuzi na wataalamu wa afya.
“Kupitia mkutano huu wa magonjwa ya moyo tumeweza kujifunza
kutoka kwa wenzetu wa mataifa mbalimbali lakini pia nao wameweza kuona ujuzi
tulionao Afrika”, alisema Dkt. Islam
Comments
Post a Comment