Waandishi wa Habari watakiwa kutumia kalamu zao kuelimisha jamii magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui
tuzo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
ya kumpongeza kwa kuwa kiongozi mwenye maono ya kuleta mabadiliko katika
matibabu ya magonjwa ya moyo Afrika. Tuzo hiyo imetolewa jana wakati wa kufunga
mkutano wa siku tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliofanyika Sea Clif
& Spa Zanzibar
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt.
Nassor Ahmed Mazrui akifundishwa jinsi ya kutoa huduma ya kuokoa maisha wakati
wa kufunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kumalizika jana katika Hoteli ya Sea
Clif & Spa Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt.
Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka
Shirika la Madaktari Afrika lililopo nchini Marekani Mazen Albaghdadi wakati wa
kufunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na kumalizika jana katika Hoteli ya Sea
Clif & Spa Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt.
Nassor Ahmed Mazrui akimpatia cheti cha kudhamini mkutano wa tatu wa kimataifa
wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naibu
Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Moyo Uganda Dkt. Peter Lwabi wakati wa kufunga
mkutano huo jana katika Hoteli ya Sea Clif & Spa Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Nassor Ahmed Mazrui akiwapatia cheti cha kudhamini mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wataalamu kutoka kampuni ya uingizaji na usambazaji wa vifaa tiba Novomed wakati wa kufunga mkutano huo jana katika Hoteli ya Sea Clif & Spa Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na washiriki wa mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa kufunga mkutano huo jana katika Hoteli ya Sea Clif & Spa Zanzibar.
Waziri wa Afya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt.
Nassor Ahmed akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu walioandaa maandiko ya
magonjwa ya moyo wakati wa kufunga mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya
moyo ulioandaliwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana katika Hoteli
ya Sea Clif & Spa Zanzibar.
Na: JKCI
*************************************************************************************************
Waandishi wa Habari watakiwa kutumia kalamu zao kusambaza
habari za kuwataka wananchi kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya hasa katika
masuala ya lishe, mtindo bora wa maisha, na kuepuka tabia bwete zinazoweza
kusababisha magonjwa ya moyo.
Rai hiyo imetolewa jana na Waziri wa Afya Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Nassor Ahmed Mazrui wakati wa kufunga mkutano wa
tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Sea
Clif & Spa Zanzibar.
Mhe. Dkt. Nassor alisema waandishi wa habari wakitumia vizuri
kalamu zao zitasaidia kupunguza magonjwa ya moyo nchini kwani magonjwa hayo ni changamoto
isiyo na mipaka hivyo ni wajibu wao kushirikiana na sekta ya afya kuhakikisha nchi
inapambana na tatizo hilo na kuokoa maisha.
“Magonjwa ya moyo ni janga linaloweza kudhibitiwa kupitia
elimu, uelewa, na ushirikiano wa kimataifa, kwa maana hiyo mkutano huo
utawawezesha wadau kubadilishana uzoefu katika kupambana na magonjwa yanayotishia
maisha ya watu wengi duniani”, alisema Mhe. Dkt. Nassor
Mhe. Dkt. Nassor alisema mkutano huo wa kipekee umeweza
kuwakutanisha wataalamu wa afya kutoka maeneo mbalimbali duniani kujadili kwa
pamoja namna ya kukuza ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa ya moyo,
hivyo na waandishi wa habari wakisaidia jamii itakuwa katika nafasi nzuri ya
kuyaepuka magonjwa ya moyo.
“Bado kuna kazi kubwa
yakufanya ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 kwani
matokeo yanaonesha kumekuwa na changamoto ya watu kutozingatia matibabu, mfano
mtu mmoja kati ya watano upande wa wagonjwa wa shinikizo la damu utumia dawa
wanne wanaobaki hawatumii dawa”, alisema Mhe. Dkt. Nassor
Aidha Mhe. Dkt. Nassor ametoa wito kwa washiriki wa mkutano
huo kuendelea kushirikiana kwa karibu katika kuendeleza tafiti, kuboresha
matibabu na kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mbali na kuboresha huduma za matibabu
ya moyo mkutano huu pia umelenga katika mkakati wa kutekeleza tiba utalii
nchini Tanzania kwani dunia nzima imeona na kujenga imani juu ya uwezo wa JKCI
katika kutoa huduma ususani matibabu ya moyo.
Dkt. Kisenge alisema mkutano huo umeudhuriwa na mataifa 25 ikiwemo Kenya, Uganda, Malawi,
Zambia, Rwanda, Amerika, Chile, Korea, China, Israel, Poland, Afrika Kusini,
Misri, Italy, Tunisia, Zimbambwe, Ujerumani, India na Uingereza.
Aliongeza kuwa kupitia mkutano huo wakuu wa Hospitali za moyo
kutoka nchi za Afrika wameweza kukutanishwa ikiwemo hospitali za moyo za Zambia,
Rwanda na Uganda.
“Wakuu wa taasisi mbalimbali za kimataifa zinazojihusisha na
matibabu ya moyo nao wameshiriki nasi ikiwemo Shirika la Save a Child Hearts la
nchini Israel Shirika la Madaktari Afrika la nchini Marekani, Chama cha
wataalamu wa moyo kutoka bara la Amerika, pamoja na Maabara ya Chuo Kikuu cha
Philips kilichopo nchini Ujerumani”,
“Lengo la kukutana kwa wakuu wa taasisi ni pamoja na
kuangalia namna ya kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya moyo kupitia
njia ya ushirikiano”, alisema Dkt. Kisenge
Naye Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Prof.
Abel Makubi aliupongeza uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kutokuwa na ubinafsi katika kushirikiana na wadau wengine kubadilisha ujuzi katika
masuala ya magonjwa ya moyo.
Prof. Makubi alisema taasisi nyingine za afya ni sehemu ya
mafanikio ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na taasisi hizo zipo tayari
kuendelea kushirikiana nao kwani wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja hasa upande
wa kinga na namna ya kukabiliana na magonjwa hayo.
“Hospitali ya Benjamini Mkapa imekuwa ikifanya kazi pamoja na
JKCI katika kuboresha huduma za magonjwa ya moyo, na tutaendelea kushirikiana
nao”, alisema Prof. Abel Makubi
Mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wenye kauli
mbiu “kuimarisha huduma za moyo barani
Afrika kupitia jitihada za pamoja” umefanyika kwa siku tatu na kumalizika jana
kwa kuwakutanisha wataalamu wa magonjwa ya moyo 424 kutoka nchi 25 ambapo kati
yao wataalamu 107 wametoka nje ya nchi na wataalamu 317 kutoka hospitali
mbalimbali nchini.
Comments
Post a Comment