Watu 249 wachunguzwa na kutibiwa moyo Zanzibar
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Happy Mabonka akimuonesha huduma zinazotolewa na taasisi hiyo Afisa Muuguzi wa Hospitali ya Magogoni Saida Sadifa wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku nne katika uwanja wa Amaani Zanzibar. Watu 249 walipata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika katika upimaji huo uliokwenda sambamba na kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali.
Hadija Said mkazi wa Daraja Bovu akimuonesha
daftari lililoandikwa dawa za moyo anazozitumia Daktari wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Dotto Sebastian wakati wa kambi maalumu ya upimaji na
matibabu ya moyo iliyofanyika katika uwanja wa Amaani Zanzibar. Watu 249 walipata huduma za uchunguzi na
matibabu ya moyo katika katika
upimaji huo uliokwenda sambamba na kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari,
Uhusiano na Itifaki wa Serikali.
Wakazi wa Zanzibar wakiwa katika foleni ya kwenda kumuona daktari wa moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika kwa siku nne katika uwanja wa Amaani Zanzibar. Watu 249 walipata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kati yao 199 walikutwa na matatizo ya moyo hii ni sawa na asilimia 80 ya watu wote walioonwa ambapo watu 77 sawa na asilimia 31 hawakuwa wanajijua kuwa na matatizo ya moyo.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Aika Nnkya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.
Dkt. Aika alisema kati ya watu 249 waliowafanyia uchunguzi watu 199 walikutwa na matatizo ya moyo hii ni sawa na asilimia 80 ya watu wote waliowaona ambapo watu 77 sawa na asilimia 31 hawakuwa wanajijua kuwa na matatizo ya moyo.
“Wagonjwa 22 ambao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuziba kwa mishipa ya damu, mfumo wa umeme wa moyo na valvu tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi yetu ili tuwafanyie uchunguzi zaidi”.
“Ninatoa wito kwa wananchi zinapotokea nafasi za upimaji kama hizo wajitokeze kwa wingi kupima afya zao kwa mfano katika kambi hii watu waliokutwa na matatizo wametibiwa na kupewa dawa za kutumia mwezi mmoja bila malipo yoyote yale” alisema Dkt. Aika.
Kwa upande wake mratibu wa kambi hiyo ya matibabu daktari bingwa wa moyo kutoka hospitali ya Rufaa Lumumba Khamis Mustafa alishukuru kuwepo kwa kambi hiyo na kusema kuwa imesogeza kwa karibu huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.
“Ninazishukuru sana Idara
za Habari maelezo kwa kuja na wazo hili katika mkutano wao kuwepo na huduma ya
upimaji na matibabu kwa wananchi kwani wataalamu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) , Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Tiba ya
Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametoa huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali”.
“Ninaomba kambi hii ya
matibabu ya kibingwa ya magonjwa mbalimbali ambayo inahusisha hospitali hizi
kubwa tatu iwe endelevu kwani inawasaidia wananchi kupata huduma za matibabu ya
kibingwa kwa wakati na bila gharama yoyote ile tofauti na ambavyo wangezifuata
Dar es Salaam”, alisema Dkt. Ndiz.
Nao wananchi waliopata
matibabu katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma walizozipata na kusema kuwa
zimwewasaidia kufahamu hali za afya ya miili yao na wengine kupata matibabu
kutokana na matatizo waliyokuwa nayo.
“Ninaishukuru Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kwa kutuletea wataalamu hawa mimi nilikuwa nikilala moyo
wangu unakwenda kasi sana baada ya kufanyiwa uchunguzi nimeambiwa moyo wangu
unashida kidogo nimepewa dawa za kwenda kutumia”, alishukuru Halima Shaaban
mkazi wa Mwera.
“Baada ya kusikia kuna
huduma za matibabu nilikuja hapa kutibiwa kwani mimi ninatatizo la mgongo na
presha , nimefanyiwa vipimo na kupewa dawa za kwenda kutumia ninashukuru sana
na ninawaomba wananchi wenzangu wachangamkie fursa hii ya matibabu pindi
inapotokea”, alisema Juma Abdala mkazi wa Makunduchi.
Huduma hiyo ya matibabu ilitolewa kwa wananchi za Zanzibar na washiriki wa kikao kazi cha 20 cha Maafisa Habari, Uhusiano na Itifaki wa Serikali kilichoandaliwa na Idara za Habari – Maelezo za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Comments
Post a Comment