Watu milioni 4.9 nchini husumbuliwa na magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimuelezea Makamu wa pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla namna wanavyofanya upasuaji wa kubadilisha
valvu ya moyo bila kufungua kifua wakati wa ufunguzi wa mkutano wa tatu wa
kimataifa wa magonjwa ya moyo uliofanyika jana mjini Zanzibar.
Afisa masoko kutoka kampuni ya Snibe Diagnostic Vonnie Feng
akimuelezea Makamu wa pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman
Abdulla huduma zinazotolewa na kampuni hiyo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa
tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliofanyika jana mjini Zanzibar.
Makamu wa pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka nchi mbalimbali walioudhuria mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika jana mjini Zanzibar.
Makamu wa pili wa Rais Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.
Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya maandalizi ya
mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wakati wa ufunguzi wa mkutano
huo uliofanyika jana mjini Zanzibar.
Na: JKCI
*******************************************************************************************
Imebainishwa kuwa magonjwa ya moyo na shinikizo la damu
huchangia vifo takribani milioni 20 kwa mwaka duniani, idadi ambayo ni sawa na
kupoteza wastani wa watu 50 kila siku.
Kwa takwimu za hapa nchini watu milioni 4.9 husumbuliwa na
magonjwa ya moyo ambapo asilimia 13 ya vifo vyote nchini hutokana na magonjwa
hayo.
Hayo yamesemwa jana na Makamu wa pili wa Rais Serikali ya
Mapinduzi Zanzibara Mhe. Hemed Suleiman Abdull akimuwakilisha Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa
mkutano wa tatu wa kimataifa wa magonjwa ya moyo uliofanyika katika Hoteli ya
Sea Clif iliyopo mjini Zanzibar
Mhe. Hemed aliwataka washiriki wa mkutano huo kushiriki na
kutumia fursa waliyoipata kujumuika pamoja kutafuta mbinu za kuzuia na
kudhibiti magonjwa ya moyo.
“Mkutano huu uwasaidie kujengeana uwezo na kuboresha nyenzo
za utendaji kazi wenu ili muweze kukabiliana na ongezeko la magonjwa
yasioyoambukiza ususani magonjwa ya moyo na mishipa ya damu”, alisema Mhe.
Hemed
Mhe. Hemed aliwataka washiriki kupitia mkutano huo kuweza
kuwa na majibu sahihi katika maeneo muhimu yenye changamoto upande wa udhibiti
wa magonjwa, ujuzi katika uchunguzi, matibabu na uendelevu wa huduma mpya
zinazopatikana nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa alioufanya
katika Taasisi hiyo pamoja na Rais Hussein Mwinyi kwa kuimarisha sekta ya afya
Zanzibar.
Dkt. Kisenge alisema JKCI ilivyo sasa ni matokeo ya safari ya
ubunifu iliyofanywa tangu mwaka 2015 safari ambayo sasa taasisi hiyo inafanya
upasuaji wa tundu dogo kwa wagonjwa 3000 na upasuaji wa kufungua kifua kwa
wagonjwa 800 kwa mwaka.
“JKCI ni miongoni mwa Taasisi bora barani Afrika kwa kutoa
huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo, sasa tunaweza kufanya
upasuaji wa kubadilisha valvu za moyo bila kufungua kifua “Tavi Procedure”, alisema Dkt. Kisenge
Dkt. Kisenge alisema kikao hicho cha magonjwa ya moyo
kitawasaidia kushirikiana na wadau kwa pamoja kupata suluhisho la kuwasaidia
wagonjwa wa moyo wanaowahitaji kutoka nchi mbalimbali duniani.
“Kupitia mkutano huu JKCI inaenda kuokoa Afrika katika
masuala ya magonjwa ya moyo kwani sasa nchi za Afrika zinatutumia katika kutoa
huduma za matibabu ya moyo kama vile Malawi, Zambia, Comora na hivi karibuni
Burkina Faso itatutumia”, alisema Dkt. Kisenge
Comments
Post a Comment