JKCI yapata tuzo utoaji huduma bora za Afya 2025 ngazi ya hospitali maalum na Taifa
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi tuzo ya mshindi wa utoaji wa huduma bora za Afya mwaka 2025 kundi la Hospitali maalumu na Taifa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa iliyohitimishwa leo jijini Dodoma.
Wananchi wa mkoa wa Dodoma wakipata elimu kuhusu magonjwa ya
moyo kutoka kwa wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
walipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya
Kitaifa yaliyohitimishwa leo jijini Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akizungumza na baadhi ya viongozi wakati wa maadhimisho ya
wiki ya Afya Kitaifa iliyomalizika leo jijini Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na mtoto Naima Kasiki aliyewahi kufanyiwa upasuaji wa moyo akiwa na miezi nane katika Taasisi hiyo pamoja na pacha wake Neyman Kasiki (Kulia) walipotembelea banda la JKCI wakati wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa leo jijini Dodoma
Na: JKCI
***********************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepata tuzo ya ushindi
wa utoaji wa huduma bora za afya kwa mwaka 2025 katika kundi la Hospitali
maalum na Taifa.
Tuzo hiyo imetolewa leo na Waziri wa Afya Mhe. Jenista
Mhagama wakati wa kufunga maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa yaliyokuwa
yakifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini
Dodoma.
Akitoa tuzo hiyo Mhe. Jenista ameipongeza Taasisi hiyo kwa
kuzingatia usafi wa maeneo ya kazi, utoaji wa huduma bingwa na bobezi, pamoja
na utoaji wa huduma bora kwa wateja (customer care services).
“Taasisi hii imezingatia usafi wa mazingira na usalama kwa
wagonjwa wanaowahudumia, nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya”, alisema
Mhe. Jenista
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema JKCI itaendelea kuboresha huduma
inazozitoa huku ikiendelea kufikisha huduma hizo kwa wananchi waliopo mikoani
kupitia kambi maalumu ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea
kuwekeza vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi yetu na kuifanya taasisi hii kuwa
kituo cha ubora Afrika Mashariki na kati katika kutoa huduma za kibingwa za
uchunguzi na matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge
Naye mkazi wa Dodoma Grace Ringo ameipongeza Taasisi hiyo kwa
kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kuokoa maisha ya watoto wanaohitaji matibabu
ya moyo.
“Taasisi hii iliweza kuokoa maisha ya mtoto wangu aliyekuwa
na matundu mawili kwenye moyo wake, walimfanyia upasuaji wa kuziba matundu hayo
mwaka 2014 akiwa na miezi nane na sasa ana miaka 11 na afya yake ipo vizuri
kabisa”, alisema Grace
Aidha Grace amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Taasisi hiyo na kuweza kusaidi
watoto kama ambavyo wakwake alisaidiwa.
Comments
Post a Comment