Singida wafikiwa na huduma za kibingwa za matibabu ya moyo
Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias Birago akitoa ushauri wa afya ya moyo kwa Nelson Mnyanyi aliyetembelea banda la
taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali
Pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Mandewa, mkoani Singida.
Katika jitihada za kuboresha huduma za afya nchini, Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za uchunguzi na elimu kwa wananchi
kuhusu njia bora za kujikinga na magonjwa ya moyo kupitia maonesho ya Kimataifa
ya Wiki ya Usamala na Afya Mahali pa Kazi.
Uchunguzi na elimu hiyo vinafanywa na Taasisi hiyo katika
viwanja vya maonesho vya Mandewa vilivyopo mkoani Singida.
Taasisi hiyo inatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo
kwa kutumia mashine za kisasa zinazoweza kugundua tatizo la mgonjwa mapema
pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya
moyo.
Huduma hizo zimekuwa zikitolewa bila gharama kama sehemu ya
kuihamasisha jamii kuwa na tabia ya kuchunguza afya lakini pia kama sehemu ya
kuhamasisha afya bora mahali pa kazi.
Aidha wananchi wanaopatikana na viashiria vya magonjwa ya
moyo wanapewa ushauri wa kitaalamu na wengine kupewa rufaa kwaajili ya matibabu
zaidi.
Maonesho hayo yamekuwa fursa kwa wakazi wa mkoa wa Singida na
mikoa ya jirani kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kuongeza
uelewa wao kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo.
Comments
Post a Comment