Utalii tiba waongeza idadi ya wagonjwa wanaotibiwa JKCI
Afisa kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adam Sembe
akimuelezea mwananchi wa Dodoma huduma za utalii tiba zinazotolewa na Taasisi
hiyo wakati wa maonesho ya kuadhimisha wiki ya afya kitaifa yanayofanyika
katika kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma.
Wananchi wa Dodoma wakipata elimu kuhusu magonjwa ya moyo
katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya
kuadhimisha wiki ya afya kitaifa yanayofanyika katika kituo cha Mikutano cha
Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma.
Na: JKCI
**********************************************************************************************
Upatikanaji wa huduma za Utalii tiba katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) umesaidia kuongeza idadi ya wagonjwa wa nje ya nchi kutoka
wagonjwa 316 mwaka 2023 hadi kufikia wagonjwa 689 mwaka 2024 wanaotibiwa na
Taasisi hiyo.
Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na
mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Benjamini wakati
wa maadhimisho ya wiki ya Afya Kitaifa inayofanyika katika viwanja vya kituo
cha Mikutano cha Jakaya Kikwete kilichopo jijini Dodoma.
Dkt. Alex alisema ukilinganisha na miaka ya nyuma kabla ya
kuanzishwa kwa kampeni za utalii tiba nchini wagonjwa waliokuwa wanafika JKCI
walikuwa kutoka nchi chache tofauti na ambavyo sasa wanapokea wagonjwa kutoka
nchi nyingi zaidi.
“Kupitia kampeni ya utalii tiba nchini JKCI sasa tunapokea
wagonjwa kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Jamhuri ya Watu wa
Comoro, Zambia, Uganda, Msumbiji, Nigeria, Congo, Ethiopia, Burundi, Siera
Leone, Zimbabwe na wengine kutoka nje ya Afrika katika nchi za Armenia, China,
Ujerumani, India, Uingereza, Ufaransa na Norway”, alisema Dkt. Alex
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Dodoma
waliotembelea banda la JKCI wamesema kuwepo kwa banda la taasisi hiyo katika
maonesho hayo kumewapa fursa adhimu ya kujifunza na kuijua vizuri taasisi hiyo.
Wananchi hao wamesema uwekezaji uliofanywa katika sekta ya
afya umesaidia kupunguza idadi ya wagonjwa kwenda nje ya nchi kufuata huduma za
kibingwa hivyo kuzitumia vizuri hospitali zilizopo nchini.
Mwanada Kimambo alisema huduma za afya nchini ziendane na
maendeleo ya sayansi na teknolojia ili utalii tiba unaofanywa na JKCI uendelee
kupata wadau wengi kutaka kutibiwa Tanzania.
“Kuna wakati nilisikia wataalamu kutoka Burkina Faso wamekuja
JKCI kujifunza, kwakweli sikuamini kama sasa Tanzania tupo kwenye kiwango cha
juu katika huduma za matibabu ya moyo hadi mataifa mengine wanakuja kujifunza
kwetu”, alisema Mwanada
Naye Ibrahimu Mwilo alisema serikali ya awamu ya sita
imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwani sasa wananchi wanapata
huduma za afya kwa urahisi kutokana na huduma hizo kupatikana hadi maeneo ya
vijijini.
Comments
Post a Comment