Majaliwa atoa wito kwa watoa huduma za afya kuzingatia maadili ya taaluma zao
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa akizungumza na madaktari wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) Arusha.
********************************************************************************************
▪ Asema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kuboresha huduma
za afya
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa mabaraza ya
kitaaluma, Chama cha Madaktari na vyama vingine vya kitaaluma kukemea
vitendo vilivyo kinyume na maadili ya taaluma na kuchafua taswira ya fani hiyo.
Ametoa wito huo leo Jumatano (Juni 18, 2025) alipomwakilisha
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari
Tanzania (MAT) na Kongamano la Kitaifa la Tiba pamoja na maadhimisho ya miaka
60 ya MAT, kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, jijini
Arusha.
”Wataalamu wote wa afya zingatieni miiko na maadili ya
taaluma zenu kwa kutoa huduma bora kwa wananchi. Kila mmoja achukue wajibu wa
kuwaonya wale wanaochafua taswira na heshima ya kada hii kwa tabia zisizofaa za
uzembe, lugha zisizo na staha, rushwa, wizi wa dawa na vifaa”
Ķuhusu jitihada za Serikali za kusogeza huduma za afya karibu
na wananchi, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imeongeza vituo vya
kutolea huduma za afya kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 12,846
sawa na ongezeko la vituo 4,297.
“Ongezeko hili la vituo limewezesha asilimia 80 ya wananchi
kupata huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano. Mpango wa serikali ni
kufikia asilimia 95 ya wananchi ifikapo mwaka 2030 watakaopata huduma karibu na
makazi yao”.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara
ya Afya imefanikisha kutekeleza kampeni maalum ya kufikisha huduma za kibingwa
na ubingwa bobezi hadi Hospitali za Halmashauri ambapo jumla ya Madaktari
Bingwa 250 walishiriki kutoa huduma katika kambi mbalimbali hapa nchini.
Kadhalika, Amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne,
Serikali imeongeza MRI kutoka saba hadi kufikia 13, CT Scan zimeongezeka kutoka
12 hadi 45, Ultrasound kutoka 476 hadi 970, Digital X-ray kutoka 147 hadi 491.
“Kadhalika ili kufanikisha uchunguzi na ufuatiliaji wa ugonjwa wa saratani,
Serikali imenunua PET CT - Scan yenye thamani ya Shilingi Bilioni 18.5”.
Ameongeza kuwa, Katika kukabiliana na athari zitokanazo na
mabadiliko ya kisera ya baadhi ya wadau wa sekta ya afya, Serikali imefanya
tathmini ya namna ya kukabiliana na hali hiyo na tayari kiasi cha shilingi
bilioni 141.9 kimetolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na bidhaa nyingine za
afya.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel
amepongeza Rais Dkt. Samia kwa kutoa kiasi cha shilingi trilioni 6.7 ambazo kwa
kiasi kikubwa zimezifanya Tanzania kuwa kinara katika sekta ya afya miongoni
mwa Mataifa mengi “kiasi hiki kimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya
nchini”.
Comments
Post a Comment