Wanaume wajitokeza kwa wingi kupima moyo Dodoma
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akimuhudumia mwananchi aliyefika katika banda la
taasisi hiyo jana kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa
Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Upendo Mwaipopo akimpima shinikizo la damu mkazi wa Dodoma aliyefika katika banda la taasisi hiyo jana kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Watu 259 wamepata huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo inayotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi ya Umma yanayofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Hayo
yamesemwa jana jijini Dodoma na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu huduma hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.
Dkt. Maucky
alisema wagonjwa waliowaona tangu kuanza
kwa maonesho hayo wengi wao ni wanaume ukilinganisha wa wanawake hali hiyo
imekuwa ni tofauti na maeneo mengine ambayo wanakwenda kutoa huduma kama hiyo ambako
idadi ya wanawake wanakuwa ni wengi zaidi.
“Kati
ya watu 259 tuliowapa huduma wanaume walikuwa 168 na wanaweka 91 mwitikio umekuwa
ni mkubwa zaidi kwa wanaume ukilinganisha na wanawake na watu tuliowaona wengi
wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, kisukari, moyo kutanuka na
shida ya valvu kutokufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Maucky.
Dkt.
Maucky alisema mgonjwa aliyekutwa na shida ya valvu ilikuwa ni mara yake ya
kwanza kufanyiwa vipimo vya moyo na hakuwa anajijua kuwa na shida, baada ya
vipimo valvu yake ilikutwa na shida na hivyo kupewa rufaa ya kwenda JKCI kwa
ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuibadilisha.
“Ninawaomba
wananchi mtumie nafasi hii kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yenu
huduma hii inatolewa bila malipo yoyote yake, tumieni siku tatu zilizobaki
katika maonesho haya kuja kupima na kupata ushauri wa jinsi ya kuepukana na
magonjwa haya”, alisisitiza Dkt. Maucky.
Kwa
upande wa wananchi waliopata huduma ya ushauri, upimaji na matibabu ya moyo
walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu afya za
mioyo yao.
“Mimi
ni mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam nilifika hapa kupata huduma katika Wizara
ya Ardhi, baada ya kusikia kuna huduma za upimaji wa moyo nimekuja kupima
nimepata huduma nzuri na ninashukuru baada ya vipimo moyo wangu uko vizuri”.
“Daktari
amenishauri niendelee kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, ninawaomba
wananchi wenzangu mjali afya zenu kwanza kabla ya vitu vingine kwa kuja kupima kwani
huduma za upimaji zinatolewa bure hulipii chochote kile”, alisema Elisafi
Kifimbo.
“Baada
ya kufika hapa na kufanyiwa vipimo nimekutwa na tatizo la uzito mkubwa,
mtaalamu wa lishe amenishauri kufanya
mazoezi na amenielekeza aina ya vyakula vya kula ili nipunguze uzito”.
“Nashukuru
huduma niliyopata ni nzuri na sijalipia kitu chochote, ninaiomba serikali itusaidie
kutoa huduma hizi mara kwa mara ili sisi ambao uwezo wetu kiuchumi ni mdogo tuweze kupata huduma za kibingwa za
matibabu ya moyo ambazo zitatupunguzia gharama ya kulipia na kuzifuata Dar es
Salaam”, alishukuru Ester Masingija mkazi wa Ihumwa.
Comments
Post a Comment