Waziri Simbachawene aipongeza JKCI kwa matibabu bure ya moyo Dodoma
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitazama valvu ya moyo wanayowekewa wagonjwa ambao valvu zao hazifanyi kazi vizuri alipotembela banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akitazama betri la moyo “Pacemaker” wanalowekewa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimia 50 alipotembela banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akimkabidhi Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene folder lenye taarifa za taasisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juma Mkomi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Mhe. George Simbachawene ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa
kutoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa kuwafuata wananchi mahali
walipo.
Pongezi
hizo amezitoa jana alipotembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya
Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park
jijini Dodoma.
Akiwa
katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Mhe. Simbachawene aliona huduma
za ushauri, upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa kwa wananchi pamoja na
vifaa visaidizi vya moyo ambavyo wanawekewa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji na
vifaa vinavyotumika katika upasuaji wa moyo.
“Ninawapongeza
kwa huduma mnayoitoa ya kuokoa maisha ya wananchi wenye shida za moyo, ninawasihi
muendelee na moyo wenu wa kujitoa ili
watu wengi zaidi wafikiwe na hudum hii na kupata matibabu mapema”, alisema Mhe.
Simbachawene.
Kwa upande
wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Ghati Chacha alisema huduma wanazozitoa katika maonesho hayo ni upimaji
wa shinikizo la damu (BP), upimaji wa kiwango cha sukari kwenye damu, upimaji
wa uwiano baina ya urefu na uzito, vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi.
“Pia
tunatoa ushauri wa kiafya kuhusiana na magonjwa ya moyo, elimu ya lishe, elimu
ya upasuaji wa moyo, elimu ya upandikizaji wa vifaa visaidizi vya moyo, elimu
ya uzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo na huduma ya utumishi na utawala”.
“Huduma hizi tunazitoa bila malipo yoyote yale, ninawaomba wananchi mtembelee banda letu ili muweze kupata huduma huduma za elimu, ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo”, alisema Ghati.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Himiza matumizi ya mifumo ya kidigilali ili kuongeza upatikanaji wa taarifa na kuchagiza uwajibikaji”.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imekuwa ikitoa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo ijulikanayo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kuwafuata wananchi mahali walipo ambapo hadi sasa wameshafika zaidi ya mikoa 20 na kuhudumia watu zaidi ya 21,324.
Comments
Post a Comment