Kambi ya matibabu ya moyo bila malipo yafanyika Arusha
Daktari Bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rose Chengo akimfanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mtoto aliyefika kupata huduma ya matibabu ya moyo katika kambi ya maalumu ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bertha Massawe akiongea na mkazi wa Arusha kuhusu magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Wananchi wa mkoa wa Arusha wakiwa katika foleni ya kusubiri huduma ya matibabu ya moyo kwenye kambi maalumu ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
********************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika kambi maalumu ya matibabu siku saba ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali inayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo jijini Arusha.
Kambi hiyo ya matibabu imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambapo huduma zinatolewa bila malipo JKCI inatoa huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo na kutoa ushauri na elimu ya lishe bora pamoja na matumizi sahihi ya dawa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha kuhusu kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce alisema lengo la ushiriki wa taasisi hiyo ni kusaidia wananchi kugundua matatizo ya moyo mapema na kuanza matibabu kwa wakati.
“Lengo letu ni kutambua matatizo ya moyo yanayowasumbua wananchi ili wapate matibabu mapema na kujua visababishi vya msingi vinavyochochea magonjwa haya hii itatusaidia kuwalinda wananchi dhidi ya madhara makubwa ya moyo hapo baadaye”, alisema Dkt. Aloyce.
Dkt. Aloyce aliongeza kuwa vifaa vinavyotumika na taasisi hiyo ni vya kisasa na vinawawezesha kubaini matatizo ya moyo kwa haraka kwa watu wa rika zote kuanzia kwa mtoto aliye tumboni kwa kumpima mama mjamzito, watoto na watu wazima.
“Wananchi wasipoteze fursa hii muhimu ambayo serikali imeandaa kwaajili yao, wajitokeze kwa wingi kupima afya za mioyo yao ili waweze kujua matatizo ya kiafya walio nayo mapema na kutapa matibabu sahihi na kwa wakati”, alisema Dkt. Aloyce.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliopata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewapunguzia gharama za kulipia matibabu hayo.
“Nimekuwa nikipata maumivu ya kifua mara kwa mara lakini sikuwa najua sababu ila leo nimepimwa na nimeelezwa hali yangu ya moyo na jinsi ya kujitunza ili nisipate matatizo ya moyo, nawashukuru madaktari wa JKCI kwa msaada huu walionipa” alisema Romani Kauki mkazi wa Simanjiro.
“Tulizoea kuona huduma za moyo zikitolewa kwa gharama kubwa lakini leo nimehudumiwa bure kabisa hii imenipa moyo wa kuendelea kuchunguza afya yangu ya moyo mara kwa mara hata kama siyo wakati wa kambi kama hizi”, alishukuru Happiness Langay mkazi wa Ngaramtoni.
Kambi hiyo ya matibabu imelenga kuwafikia wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani kwa kuwapatia huduma bora za afya bila gharama yoyote ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya kuboresha huduma kwa wananchi.
Comments
Post a Comment