Watu 506 wapimwa moyo Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
Mtaalamu wa lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo akitoa elimu ya lishe kwa wananchi waliofika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika jana katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Afisa Tawala wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Adila Musa akimweza mwananchi huduma zinazotolewa na taasisi hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika jana katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mwananchi aliyefika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo zilizokuwa zinatolewa kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika jana katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
*****************************************************************************************************************************************************************************************************
Watu 506 wamepata huduma ya uchunguzi wa moyo bila
malipo katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika jana
katika Viwanja vya ChinangalI Park jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa jana na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu huduma ya upimaji waliyoitoa katika Maadhimisho hayo.
Dkt. Maucky alisema kati ya watu waliowapima 306 sawa na
asilimia 60 walikuwa na matatizo mbalimbali ya moyo yakiwemo ya shinikizo la
juu la damu, mfumo wa umeme wa moyo, mishipa ya damu kuziba na valvu kutokufanya
kazi vizuri.
“Watu 291 tuliwafanyia kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya
kazi ambapo watu 22 tuliowakuta na matatizo ya moyo yaliyohitaji uchunguzi
zaidi na matibabu ya kibingwa tumewapa rufaa ya kuja kutibiwa katika taasisi
yetu iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam”.
“Kuna ambao tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu
hawa tumewapa ushauri wa aina gani ya dawa za kutumia ambazo zitawasaidia pia tumewapa
ushauri wa kufuata mtindo bora wa maisha”, alisema Dkt.Maucky.
Dkt. Maucky alitoa wito kwa wananchi kufuata matumizi sahihi
ya dawa wanazoandikiwa na wataalamu wa afya kwani kuna baadhi ya watu
waliokutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu walikuwa wameacha kutumia dawa
kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
Naye mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Emmanuel Lingindo alisema watu walioonwa katika banda hilo
walipewa ushauri wa lishe bora na kufuata mtindo bora wa maisha ambao
utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo.
“Asilimia 90 kati ya watu 195 niliowapa ushauri wa mtu mmoja
mmoja walikuwa na uzito mkubwa ukilinganisha na urefu wao nimewashauri vitu vya
kufanya ikiwemo aina ya vyakula ambayo watavitumia pamoja kufanya mazoezi ili
wapunguze uzito”.
“Ni muhimu watu wakafuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kula vyakula bora, kutotumia bidhaa aina ya tumbaku na kutokunywa pombe kupitiliza kwa kufanya hivi wataweza kujiepusha na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, alisema Lingindo.
Comments
Post a Comment