Bodi mpya ya ALMC–JKCI kuchochea maboresho ya huduma za Moyo Kaskazini
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini (DKAK) Dkt. Godson Abel Mollel akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kilichofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Katibu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK) Mwl. Solomon Loshilu Sambweti akizungumza wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ALMC.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ALMC.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK) Dkt. Godson Abel Mollel akisaini kitabu cha wageni alipotembelea hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kwaajili ya kufungua kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa ALMC ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
******************************************************************************************************************************************************************************************************************
Kikao cha kwanza cha Bodi ya Wakurugenzi wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika kuboresha huduma za moyo Kanda ya Kaskazini.
Kikao hicho
kililenga kuweka mkakati wa kuhakikisha huduma za tiba zinakuwa bora zaidi na
kuimarisha imani ya wananchi katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati akifungua
kikao hicho jijini Arusha, Askofu wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati (DKAK)
Dkt. Godson Abel Mollel alisema hatua hiyo ni ishara ya mwanzo mpya wa
kuimarisha huduma za moyo kupitia ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili.
Askofu
Dkt. Mollel alisema bodi hiyo mpya yenye wajumbe sita imeundwa kwa uwiano wa
pande zote mbili, ambapo wajumbe watatu wanatoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) na watatu kutoka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ikiwa
na jukumu la kusimamia menejimenti na mwelekeo wa kimkakati wa ushirikiano huo.
“Ushirikiano
kati ya JKCI na ALMC ni baraka kubwa kwa wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
Kupitia bodi hii mpya tunaweka msingi imara wa kuboresha huduma za moyo,
kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya zenye
ubora na utu. Tunaiomba jamii iendelee kuunga mkono jitihada hizi kwa manufaa
ya taifa letu.”
“Tunaishukuru
sana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwepo kwa ushirikiano huu
kati ya JKCI na ALMC, tunamatumaini makubwa kuwa huduma zitakuwa bora zaidi kwa
manufaa ya wananchi,”alisema Askofu Dkt. Mollel.
Askofu
Dkt. Mollel alisema kupitia bodi hiyo, JKCI na ALMC wanatarajia kuimarisha
zaidi huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo,
kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji
wa huduma ili wananchi wapate tiba bora kwa wakati.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa
JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema bodi hiyo itakuwa chombo muhimu cha usimamizi
kitakachohakikisha huduma za afya zinazotolewa na hospitali hiyo zinakuwa bora
zaidi kwa manufaa ya wananchi.
“Ushirikiano kati ya JKCI na ALMC ni
hatua muhimu katika kuhakikisha tunatoa huduma bora za afya. Bodi hii itasimamia
menejimenti ya hospitali hii ili iweze kutoa huduma za kiwango cha juu cha
kimataifa na za kipekee kwa wananchi,” alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari
bingwa wa moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba aliongeza
kuwa lengo la ushirikiano huo ni kuifanya ALMC
kuwa kituo cha mfano katika
utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali
yakiwemo ya moyo Afrika Mashariki.
“Tunaamini kupitia ushirikiano huu
tutapata ithibati ya kimataifa, jambo litakaloongeza imani ya wananchi katika
kupata huduma za afya zenye ubora wa hali ya juu,” alisisitiza.
Mjumbe wa bodi hiyo Tosky Hans alisema
kikao cha kwanza cha bodi hiyo kimeweka mikakati mahsusi ya kuboresha huduma za
matibabu katika hospitali hiyo na kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora
zaidi.
“Tumeazimia kuifanya hospitali hii
kuwa kituo cha mfano hususan katika huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo
ambazo hapo awali zilikuwa na changamoto katika mkoa wetu wa Arusha,
tutahakikisha huduma
hizi zinawafikia wananchi wengi zaidi karibu na walipo, bila kulazimika
kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo”, alisema Hans.
Naye mjumbe mwingine wa bodi hiyo,
Prof. Rogate Mshana alisisitiza umuhimu
wa kuimarisha elimu na huduma za moyo kwa manufaa ya wananchi wa Kanda ya
Kaskazini na taifa kwa ujumla.
“Tumepewa dhamana ya kusimamia
menejimenti mpya ili kuinua elimu na huduma za moyo. Huduma hizi zitakuwa na
mchango mkubwa hata katika matukio makubwa ya kitaifa kama mashindano ya
AFCON,” alisema Dkt. Mshana.
Bodi hiyo mpya inaundwa na wajumbe watatu kutoka upande wa Serikali kupitia JKCI na watatu kutoka Kanisa la KKKT. Itakuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli za pamoja za hospitali hizo kwa lengo la kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa Watanzania na wananchi kutoka mataifa jirani.
Comments
Post a Comment