Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi akiwasalimia wanachi wa mkoa wa Arusha
waliofika kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali zilizokuwa zinatolewa katika hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi akimsalimia mkazi wa Arusha aliyefika
kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center
(ALMC). Naibu Waziri amefunga kambi maalum ya upimaji na matibabu ya magonjwa
mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika ALMC ambayo inasimamiwa na Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Afisa Muuguzi Msaidizi kutoka wodi ya Watoto Njiti (NICU) katika hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Centre (ALMC) Angel Pallangyo akimueleza Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt.
Florence Samizi kuhusu vifaa vyakisasa vinavyosaidia kuwatunza Watoto
waliozaliwa kabla ya muda (watoto njiti) katika hospitali ya Arusha Lutheran
Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi akizungumza na wananchi wa mkoa wa
Arusha waliofika kupata huduma za uchunguzi wa afya wakati wa kufunga kambi maalum
ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo iliyofanyika Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi, Mkurugenji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Kaskazini Kati Dkt. Godson Abel Mollel na baadhi ya wafanyakazi wa JKCI na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa kambi maalum ya upimaji na
matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika ALMC ambayo
inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
.JPG)
Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Florence Samizi akipokea ua kutoka kwa mfanyakazi wa
hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Mourine Kivuyo alipotembelea
hospitali hiyo hivi karibuni kwaajili
ya kufunga kambi maalum ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali
yakiwemo ya moyo iliyofanyika ALMC ambayo inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI).
************************************************************************************************************************************************************************************************************************
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Florence Samizi, amewahimiza Watanzania kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote, akisema hatua hiyo ni ngao muhimu ya kulinda familia dhidi ya mshtuko wa kifedha unaotokana na magonjwa yanayohitaji matibabu ya muda mrefu au ya kibingwa.
Dkt. Samizi alisema kujiunga na bima hiyo kutawawezesha wananchi kupata huduma za afya kwa wakati na kwa urahisi, badala ya kutegemea michango ya dharura kila inapojitokeza changamoto ya kiafya hali ambayo imekuwa ikiathiri ustawi wa familia nyingi nchini.
Alitoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa hafla ya kufunga kambi maalum ya upimaji wa afya bure, iliyoendeshwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya a Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo inasimamiwa na taasisi hiyo.
Akizungumzia hali ya afya duniani, Dkt. Samizi alisema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa zaidi ya vifo milioni 17.5, sawa na asilimia 32 ya vifo vyote duniani, husababishwa na magonjwa ya moyo. Aliongeza kuwa takwimu za hapa nchini zinaonyesha Mkoa wa Arusha kuwa miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya kiafya, hususan magonjwa yasiyoambukiza.
“Ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kuzingatia lishe bora na kuepuka tabia hatarishi ili kujikinga na magonjwa haya,” alisema.
Alibainisha kuwa magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani yameendelea kuwa changamoto kubwa ya afya duniani, yakichangia kwa kiasi kikubwa vifo na mzigo wa kiafya katika jamii.
“Serikali imejipanga kuboresha huduma za afya nchini. Hivyo, nawahimiza wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote ili pale wanapougua wapate matibabu kwa urahisi,” alisema, huku akiipongeza JKCI na ALMC kwa kuendelea kutoa huduma za kisasa, ikiwemo huduma za watoto njiti.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na hospitali za rufaa nchini ili kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza programu ya Tiba Mkoba, ambayo imesogeza huduma za kibingwa na bobezi karibu zaidi na wananchi,” alisema.
Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dkt. Godson Abel, aliishukuru serikali kwa kukubali kushirikiana na dayosisi hiyo katika uendeshaji wa Hospitali ya ALMC akisema ushirikiano huo utaongeza ufanisi na kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Katika kambi hiyo ya upimaji wa afya bure, wagonjwa zaidi ya 3,000 wakiwemo watu wazima na watoto walipatiwa huduma, sawa na wastani wa wagonjwa 290 hadi 300 kwa siku kuanzia Desemba 29, 2025 hadi Januari 9, 2026. Aidha, wagonjwa 65 walifanyiwa uchunguzi wa awali kwa ajili ya upasuaji, ambapo wagonjwa tisa walifanyiwa upasuaji mkubwa hospitalini hapo.
Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwashukuru wadau wa sekta ya afya kutoka Taasisi ya Pacific Diagnostic Ltd, kwa kutoa mashine kubwa ya uchunguzi wa afya (ultrasound) yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.15 itakayosaidia uchunguzi wa viungo mbalimbali ikiwemo utumbo, mishipa ya damu na moyo, pamoja na kifaa cha kupima mapigo ya moyo na kiwango cha hewa ya oksijeni mwilini.
Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Huzefa Adamali alisema mashine hiyo imetolewa kwa lengo la kusaidia jamii kupata huduma bora na za kisasa za afya kwa urahisi zaidi.
Comments
Post a Comment