Washiriki 600 kutoka mataifa 60 kukutana Dar kwa mkutano wa kimataifa wa moyo - CardioTan Imaging 2026
Mwenyekiti wa Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026,Iddi Lemah akiwaeleza waandishi wa habari namna mkutano huo utakavyofanyika wakati wa hafla fupi ya kuutambulisha mkutano huo uliofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza kuhusu Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026, utakaofanyika mwezi Juni mwaka huu wakati wa hafla fupi ya kuukutanisha mkutano huo iliyofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026na wafanyakazi wa Taasisi hiyo baada ya kumalizika kwa hafla fupi ya kuutambulisha mkutano huo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wadau wa afya wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akiutambulisha Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo – CardioTan Imaging 2026, katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
**************************************************************************************************************************************************************************************************
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika tarehe 4 hadi 6 mwezi Juni 2026 katika Ukumbi wa Blue Sapphire, Mbezi Beach jijini Dar es
Salaam, ukilenga
kuwakutanisha wataalamu wa afya, watafiti na wadau wa sekta ya moyo kutoka
sehemu mbalimbali duniani ili kujadili maendeleo ya kisayansi na matumizi ya
teknolojia ya kisasa katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati
wa mkutano wa kuutambulisha mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter
Kisenge alisema mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kuwajengea
uwezo wataalamu wa afya katika matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo akiliunde (Artificial
Intelligence – AI) na mbinu bunifu za uchunguzi wa moyo.
“Mkutano
wa CardioTan 2026 – CardioTan Imaging 2026, utakuwa fursa muhimu kwa wataalamu wa
afya kupata ujuzi wa kisasa katika uchunguzi wa moyo na vipimo vya kitaalamu
kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa mkutano huo pia utakuwa na mchango mkubwa katika
maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, kwa kuwa utaweka mkazo katika eneo la
Sports Cardiology
(Afya ya moyo katika michezo), jambo litakalowasaidia wataalamu wa afya kujiandaa kukabiliana na
changamoto za kiafya kwa wanamichezo na jamii kwa ujumla.
“Kwa
kuwaleta pamoja wataalamu wa ndani na wa kimataifa, tunajenga uwezo wa kitaifa
wa kushughulikia changamoto za afya ya moyo kwa kutumia mbinu za kisasa,”
aliongeza.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa JKCI na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kisayansi ya mkutano huo, Dkt. Tatizo Waane alisema mkutano
huo umejikita zaidi katika kuangazia umuhimu wa uchunguzi wa kina wa magonjwa
ya moyo kwa kutumia teknolojia za kisasa.
“Ili
mgonjwa apate tiba sahihi, lazima uchunguzi uwe wa kina na wa kitaalamu.
Kupitia mkutano huu, tutajadili na kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu bora za
kisasa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo,” alisema Dkt. Waane.
Naye
Mjumbe wa Baraza la
Mionzi Tanzania, Catherine Malika, akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Baraza hilo, aliwataka
wataalamu wa afya nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo ili
kuongeza ujuzi wao wa matumizi ya teknolojia za kisasa.
“Serikali
ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
imewekeza kwa kiasi kikubwa katika vifaa tiba vya kisasa kuanzia ngazi ya
zahanati hadi hospitali. Mkutano huu ni fursa ya kuhakikisha vifaa hivyo
vinatumika kwa ufanisi na weledi,” alisema Catherine.
Kwa
upande wake Mkuu wa Kitengo cha Vipimo vya
Moyo wa JKCI na mwanzilishi wa Chama cha Vipimo vya Moyo Tanzania (TES), Dkt.
Engarasiya Kifai, alisema mkutano huo utaongeza wigo wa maarifa
kwa wataalamu wa ndani na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya
kimataifa ya elimu ya afya ya moyo.
“Mataifa
mengi yaliyoendelea barani Ulaya na Amerika yamepiga hatua kubwa kupitia
mikutano ya kitaaluma kama hii. Kupitia CardioTan Imaging 2026, nasi tunaendelea
kujifunza na kujenga uwezo kwa manufaa ya wagonjwa wetu,” alisema Dkt.
Engarasiya.
Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Moyo wa mwaka 2026 una kauli
mbiu isemayo “Uchunguzi Mahiri wa Moyo, kwa Moyo Imara”.
Mkutano huo wa Kimataifa wa magonjwa ya moyo ni wa nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kitaaluma litakaloikutanisha dunia jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maendeleo ya huduma za moyo.
.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)
Comments
Post a Comment