Taasisi nne za Afya zashirikiana kuboresha huduma kwa wagonjwa

Wakurugenzi Watendaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Delilah Kimambo, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Balozi Ulisubisya na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kikao cha ujirani mwema kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma kilichofanyika leo katika Ukumbi wa MOI iliyopo jijini Dar es Salaam.

Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakisikiliza wakati wa kikao cha ujirani mwema kati ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma kilichofanyika leo katika Ukumbi wa MOI iliyopo jijini Dar es Salaam.


Wakurugenzi Watendaji kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Delilah Kimambo, Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Balozi Ulisubisya na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Taasisi hizo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha ujirani mwema kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma kilichofanyika leo katika Ukumbi wa MOI iliyopo jijini Dar es Salaam.

***************************************************************************************

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) zimefanya kikao cha ujirani mwema leo Ijumaa, Januari 23, 2026 jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kikao hicho kimewaleta pamoja wakuu wa taasisi hizo na baadhi ya viongozi wa menejimenti, ambapo waliangalia kwa kina masuala ya uratibu wa huduma, matumizi ya miundombinu ya pamoja na uimarishaji wa mawasiliano kati ya taasisi.

Wajumbe wameweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuboresha huduma kwa wagonjwa, hususan wale wanaohudumiwa katika taasisi jirani.

"Kwa kuwa taasisi zetu zipo eneo moja na wagonjwa wengi wanahitaji huduma zinazohusiana, ni lazima tushirikiane kwa karibu ili kuhakikisha wanapata huduma kwa wakati na kwa ufanisi," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya.

Dkt. Peter Kisenge ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI alisema  kikao hicho kimewapa fursa ya kujadili changamoto kwa uwazi na kuweka mikakati bora ya kuzitatua.

"Tumekubaliana kuimarisha mawasiliano na uratibu wa huduma ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa na kuongeza ufanisi katika matumizi ya rasilimali zilizopo," alisema Dkt. Kisenge.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo alisema kwa kushirikiana kama taasisi jirani, wataweza kubadilishana uzoefu, kuboresha mifumo ya rufaa na kuhakikisha mgonjwa anapata huduma sahihi kwa wakati unaostahili.

Aidha Makamu Mkuu wa MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa alisisitiza kuwa chuo hicho kinaendelea kuthamini ushirikiano na taasisi jirani, jambo linalowawezesha kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya, kufanya tafiti kwa pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za vitendo.

Vikao hivi vya ujirani mwema hufanyika mara mbili kwa mwaka ambapo kikao kijacho kitafanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo