RC Makala awaalika wakazi wa Arusha kupima Afya bure ALMC
Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akimsikiliza mkazi wa Arusha aliyefika Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika ALMC.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Emmanuel Lingindo akitoa elimu ya lishe kwa wakazi wa Arusha waliofika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo zinazotolewa katika kambi ya matibabu inayofanyika jijini Arusha.
Akizungumza leo wakati wa mazungumzo yake na
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge, aliyemtembelea ofisini kwake Mhe.Makala alisema kambi hiyo ni hatua
chanya kwa wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani kwani imepunguza ulazima wa
wananchi kufuata huduma za matibabu mbali hususan jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo ya matibabu inatekelezwa na
wataalamu wa JKCI kufuatia mkataba wa ushirikiano kati ya JKCI na Hospitali ya
ALMC, unaolenga kusogeza huduma za kibingwa za magonjwa ya moyo pamoja na
huduma nyingine maalum karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini.
“Kuwepo kwa kambi hii ni faida kubwa kwa
wananchi wetu kwani watapata nafasi ya kupata huduma kwa urahisi bila usumbufu
wa kusafiri umbali mrefu,” alisema Mhe. Makala.
Aliongeza kuwa uamuzi wa JKCI kuisimamia
Hospitali ya ALMC kwa kipindi cha miaka 20 utaongeza wigo wa upatikanaji wa
huduma za afya, ikiwemo kuwahudumia wageni kutoka nje ya nchi wanaohitaji
matibabu hatua itakayochangia kukuza utalii tiba katika Mkoa wa Arusha.
Mhe. Makala alisema Serikali ya Mkoa
itaendelea kushirikiana na ALMC pamoja na wadau wengine wa sekta ya afya ili
kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya
Serikali na mashirika ya dini katika utoaji wa huduma za afya umeanza muda
mrefu na umeleta mafanikio makubwa.
Aidha, aliipongeza JKCI kwa kujitoa kwa jamii
kwa kutoa huduma kwa wananchi wengi bila malipo, pamoja na kufanya maboresho ya
miundombinu na huduma zinazolenga kuongeza ufanisi na ubora wa huduma za afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema tangu kuanza kwa kambi hiyo ya
matibabu inayotolewa bila malipo yoyote jumla ya wananchi 500 wakiwemo watu
wazima na watoto wamepata huduma za uchunguzi na matibabu.
Alisema kati ya wagonjwa hao 15 wamepata rufaa
ya kwenda JKCI jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi, huku watoto 36
wakifanyiwa uchunguzi wa moyo ambapo watoto watatu kati yao wanatarajiwa
kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuziba matundu ya moyo.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa
Magonjwa ya Moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba alisema
kambi hiyo inalenga kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ya
moyo, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kibingwa karibu na maeneo yao
bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Akizungumza kuhusu kuanza rasmi kwa usimamizi
wa JKCI katika Hospitali ya ALMC, Dkt. Kisenge aliwaomba wanahabari na wahariri
kujitokeza Januari Mosi, 2026 kupima afya ya moyo bila malipo, akisisitiza kuwa
wao ni wadau muhimu katika kutoa elimu ya afya kwa jamii.
“Tunawaalika wanahabari wa Arusha waje
kujionea wenyewe kwa vitendo huduma zinazotolewa. Hospitali ya ALMC ni kitovu
cha huduma za matibabu ya moyo na ni kivutio kikubwa cha utalii tiba,” alisema.
Alibainisha kuwa kuanzia Januari Mosi, 2026
JKCI itaanza rasmi kuendesha Hospitali ya ALMC kwa kipindi cha miaka 20, ambapo
mitambo na mashine za kisasa zitasimikwa sambamba na matumizi ya teknolojia ya
akili unde (Artificial Intelligence) katika kuimarisha huduma za afya.
Dkt. Kisenge alisema lengo kuu la ushirikiano
huo ni kusogeza huduma za moyo karibu na wananchi wa Kanda ya Kaskazini,
ikiwemo matumizi ya kifaa cha Dozee, shuka maalum inayomwezesha mgonjwa
kufuatiliwa hali yake ya kiafya akiwa nyumbani ndani ya siku saba baada ya
kufanyiwa upasuaji.
“Kwa kuwa JKCI itakuwa inaendesha hospitali
hii, tutafungua na kuimarisha huduma za dharura pamoja na kusimika mtambo wa moyo,
na matarajio yetu ni kwamba ndani ya miaka miwili ijayo tutaanza kufanya
upasuaji wa moyo hapa hapa ALMC,” alisema.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo inalenga kuwa hospitali ya kimataifa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu itakayowezesha kufuatilia mwenendo wa afya za wagonjwa hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Comments
Post a Comment