JKCI, UDSM wazalisha mashujaa wa kuokoa maisha Afrika
Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Tafiti Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM) Dkt. Leonald Binamungu akimkabidhi zawadi muuguzi ambaye
amehitimu mafunzo ya miezi sita ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura na mahututi
kutoka nchini Rwanda Manirakiza Frederick wakati wa hafla fupi ya kuhitimisha
mafunzo hayo leo katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam. Jumla ya
wauguzi 14 kutoka nchi za Tanzania, Zambia na Rwanda wamehitimu mafunzo hayo.
Picha na: Khamisi Musa
***********************************************************************************************************
Wahitimu wa mafunzo bobezi ya kuwahudumia
wagonjwa wa dharura na mahututi watu wazima na watoto wametakiwa kutumia
maarifa waliyoyapata kama silaha ya kuokoa maisha ya wagonjwa bila kujali hali
zao za kiuchumi au kijamii.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa
Upasuaji wa Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya
alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Peter wakati
wa mahafali ya sita ya programu hiyo ya miezi sita, yanayoendeshwa kwa
ushirikiano kati ya JKCI na Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM).
Dkt. Angela ambaye pia ni daktari bingwa wa
usingizi na wagonjwa mahututi alisema programu hiyo inayotolewa kwa Wauguzi imekuwa
chachu muhimu ya kuimarisha ubora wa huduma za afya hasa katika maeneo ya
wagonjwa mahututi na wa dharura, ndani na nje ya Tanzania.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika
sekta ya afya, hususan katika kuendeleza wataalamu na kuimarisha vifaa tiba.
Ninyi ni zao la uwekezaji huu. Fanyeni kazi kwa ujasiri, jifunzeni kila siku na
muwe tayari kujitolea kuokoa maisha ya wagonjwa,” alisema Dkt. Angela.
Aliongeza kuwa programu hiyo imewajengea uwezo
wauguzi kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Zambia na Rwanda, hali inayoonesha kuimarika kwa ushirikiano wa
kikanda katika kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Idara ya Utafiti wa UDSM Dkt. Leonard Binamungu alisema
chuo hicho kinajivunia ushirikiano wake na JKCI alisema katika kozi hiyo UDSM hutoa mafunzo ya nadharia huku JKCI
ikitoa mafunzo ya vitendo kwa viwango vya juu vya kitaalamu.
“Ninawapongeza wahitimu 14 mliomaliza mafunzo
haya ambapo wanne wametoka nchini Zambia,
Tanzania wanne na Rwanda sita. Nendeni mkawahudumie wananchi kwa weledi, muwe
mfano wa kuigwa katika nchi zenu na muendelee kuitangaza Tanzania kama kitovu
cha huduma bora za afya,” alisema Dkt. Binamungu.
Naye Mratibu wa Mafunzo hayo Afisa Muuguzi wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI),
Joshua Ogutu alisema kozi hiyo ni ya miezi sita ambapo wahitimmu hao
wamefundishwa jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi kwa
watu wazima na watoto.
“Wakufunzi hawa wamejifunza jinsi ya kutoa
huduma kwa wagonjwa wa dharura na mahututi watu wazima na watoto ambao wamefanyiwa upasuaji wa moyo, mafunzo ya Cathlab na jinsi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaosafishwa
damu (Dialysis) ambao figo zao hazifanyi kazi vizuri”, alisema Ogutu.
Nao wahitimu waliomaliza mafunzo hayo
walieleza kuridhishwa na ubora wa mafunzo waliyopewa huku wakiahidi kuyatumia
kuboresha huduma kwa wananchi.
Afisa Muugunzi kutoka Hospitali ya Moyo Zambia
Emanuel Lusale, aliwashukuru wakufunzi
wa kozi hiyo kutoka JKCI na UDSM na kusema kuwa wamepata
maarifa na kujiamini zaidi na wamejipanga kutoa huduma bora kwa wagonjwa wanaowahudumia.
Naye Afisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya
ya Lushoto Magreth Mushi alisema
mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa kitaaluma.
“Tunamshukuru Mungu kwa mafanikio haya.
Tulianza 14 na tumemaliza wote 14. Mafunzo haya yataboresha kwa kiasi kikubwa
utoaji wa huduma kwa wagonjwa wetu,” alisema.
Programu hii inaendelea kuthibitisha mchango
mkubwa wa JKCI na UDSM katika kujenga rasilimali watu bora kwa sekta ya afya na
kuimarisha ubora wa huduma za tiba ndani na nje ya nchi.


Comments
Post a Comment