DC Arusha aongoza kwa vitendo: Apima moyo, Ahamasisha Bima ya Afya kwa wananchi
Madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) wakifanya upasuaji wa kutengeneza njia za kusafisha figo (Arterial-Venous Fistula) katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika ALMC iliyopo jijini Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimsikiliza mkazi wa Arusha aliyefika Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali inayofanyika ALMC.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI Dkt. Tatizo Waane na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI Salehe Mwinchete wakati wa kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya moyo inayofanyika Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC).
******************************************************************************************************************************************************************************************
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Joseph Mkude,
amesisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na bima ya afya ili waweze kupata
huduma za matibabu kwa urahisi na kwa wakati huku akibainisha kuwa bima ya afya
ni nguzo muhimu katika kufanikisha lengo la afya kwa wote.
Mhe. Mkude alitoa kauli hiyo jana
baada ya kupima afya yake katika kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa
mbalimbali inayotekelezwa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo kwa sasa
inasimamiwa na JKCI.
Alisisitiza
kuwa bima ya afya ina mchango mkubwa katika kuwezesha wananchi kupata matibabu
ya kibingwa ikiwemo huduma za magonjwa ya moyo ambazo mara nyingi hugharimu
fedha nyingi endapo mgonjwa atalazimika kujilipia binafsi. Alieleza kuwa
kupitia bima ya afya, wananchi hupata fursa ya kufanyiwa vipimo vya kina,
kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa na kuanza matibabu kwa
wakati bila kikwazo cha gharama.
“Kujiunga
na bima ya afya kunalinda familia dhidi ya mshtuko wa kifedha unaoweza
kujitokeza pindi mmoja wao anapokumbwa na ugonjwa unaohitaji matibabu ya muda
mrefu au ya kibingwa, ninatoa wito kwa jamii kuchukua hatua mapema kwa kujiunga
na mifumo ya bima ya afya. Katika wilaya ya Arusha tumezindua mpango wa mafunzo
katika ngazi ya wilaya, kata na mitaa”, alisema Mhe. Mkude.
Akizungumzia kambi hiyo ya
matibabu, alisema ni fursa adhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na maeneo ya
jirani kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa bila kulazimika
kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam au nje ya nchi, hali ambayo awali
ilikuwa ikiigharimu familia nyingi fedha na muda mwingi.
Aidha,
alisema amefika ALMC kupima afya ya moyo wake akiwa pamoja na wanafamilia wake,
akiwahimiza wananchi kuutumia mwanzo wa mwaka 2026 kama chachu ya kuzingatia na
kuboresha afya zao.
Naye
Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maximilian Iraghe, aliipongeza kambi hiyo huku akisema
itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kusafiri
kwenda kutafuta huduma za kibingwa nje ya mkoa.
Alisema
amehudhuria kambi hiyo akiwa ameambatana na madiwani wa kata za Jiji la Arusha
baada ya kuwahamasisha viongozi hao kujitathmini kiafya ili waweze kuwahudumia
wananchi kwa ufanisi. Alifananisha vifaa vinavyotumika katika kambi hiyo na
vile alivyoviona alipowahi kupata matibabu nchini India, akisema havina tofauti
kwa ubora.
Kwa
upande wake, Diwani wa Viti Maalumu wa Jiji la Arusha, Minata Salastule,
alisema ameridhishwa na huduma alizopata katika kambi hiyo, huku akiwahimiza
wananchi kutumia fursa hiyo kupima afya zao. Alieleza kuwa vipimo vinatolewa
kwa haraka, havichukui muda mrefu na vinamwezesha mgonjwa kupata ushauri wa
kitaalamu na kurejea nyumbani mapema.
Aliongeza
kuwa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya inapaswa kuendelea kutolewa kwa
wananchi ili wengi zaidi wajiunge, kwani bima huwasaidia kupata huduma hata
pale wanapokosa fedha taslimu. Alishukuru juhudi za JKCI na ALMC kwa kusogeza
huduma za kibingwa karibu na wananchi wa Arusha.
Kwa
upande wao waandishi wa habari waliopata nafasi ya kupima afya zao katika kambi
hiyo walisema mara nyingi huwa mstari wa mbele kuripoti masuala ya afya lakini
hujisahau wao wenyewe. Walitoa wito kwa waandishi wenzao na wananchi kwa ujumla
kujitokeza kupima afya, hususan ya moyo ili kulinda uhai wao na kuendelea
kuitumikia jamii.
Mwandishi wa Habari wa ITV, Arnord Rweyemamu aliiomba Serikali na wadau wa sekta ya afya kuendelea kusogeza huduma za kibingwa hadi maeneo ya vijijini, ambako wananchi wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma hizo huku akisisitiza kuwa afya njema ni msingi wa maendeleo ya jamii.
Comments
Post a Comment