JKCI yapanga kuifanya ALMC kitovu cha huduma za Moyo Afrika
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na wazabuni wa dawa za binadamu, vifaa tiba na vitendanishi katika kikao cha kuimarisha uhusiano na ushirikiano kilichofanyika leo katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo inasimamiwa na JKCI.
Wazabuni wa dawa za binadamu, vifaa tiba na vitendanishi wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kikao chao cha kuimarisha uhusiano na ushirikiano kilichofanyika leo katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambayo inasimamiwa na JKCI.
**************************************************************************************************************************************************************************************************
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge amesema taasisi hiyo imejipanga kuimarisha huduma za matibabu ya moyo katika Kanda ya Kaskazini pamoja na huduma nyingine zinazotolewa katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) kwa lengo la kuifanya hospitali hiyo kuwa kituo cha mfano barani Afrika katika utoaji wa huduma za moyo.
Dkt. Kisenge ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wazabuni wa dawa za binadamu, vifaa tiba na vitendanishi katika
kikao kilichofanyika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ambapo
alisema mafanikio ya taasisi yoyote ya tiba yanategemea uwajibikaji wa pamoja
wa wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa utoaji huduma.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa
ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishiba ya damu ya moyo iliyoziba aliwaomba
wazabuni hao kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo ili kuhakikisha wagonjwa
wanapata huduma bora na kwa wakati huku akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni
nguzo muhimu ya kufanikisha utendaji wa ALMC.
“Kwa
sasa JKCI inaisimamia ALMC na tayari imeanza kufanya maboresho katika maeneo
mbalimbali ya huduma na mifumo ya kazi ili kuhakikisha huduma za moyo na
magonjwa mengine zinatolewa kwa viwango vya juu vya kitaalamu, mafanikio ya hospitali
hii yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa pamoja kati ya wafanyakazi,
wazabuni na wadau wote wa sekta ya afya”, alisema Dkt. Kisenge.
Akizungumzia hatua za baadaye Dkt. Kisenge alisema ALMC itaanza
kutoa huduma za kibingwa zaidi ikiwemo uwepo wa maabara ya uchunguzi na
matibabu ya mishipa ya moyo (Cath Lab)
pamoja na upasuaji wa kufungua kifua hatua itakayopunguza rufaa za wagonjwa
kwenda nje ya mkoa na nchi sambamba na kuimarisha dhana ya Tanzania kuwa kitovu
cha utalii wa matibabu barani Afrika.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) Bunare Daniel alisema watashirikiana na wazabuni hao ili upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na
vitendanishi unakuwa
wa haraka na wa uhakika. Kila hatua watakayoichukuwa italenga kuondoa
ucheleweshaji katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
“Ushirikiano
wetu na nyinyi ni muhimu sana ili wagonjwa wapate matibabu ya haraka, salama na
ya ubora wa juu. Tunafanya
kazi kwa pamoja kuhakikisha kila mgonjwa anapata huduma bila kuchelewa au
kukosa vifaa muhimu”,
“Tunawahimiza wadau wote kushirikiana nasi kwa karibu ili huduma za moyo na
magonjwa mengine ziwe bora zaidi, huku tukihakikisha kila hatua katika upatikanaji wa vifaa
inafanyika kwa uwazi, haraka na kwa ufanisi”, alisema Bunare.
Kwa upande wao wazabuni hao
waliushukuru uongozi wa JKCI kwa kuitisha kikao hicho huku wakisema kimewapa
fursa ya kubadilishana mawazo, kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha
ushirikiano wao na taasisi hiyo katika kuboresha huduma za matibabu.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara kutoka Pacific Diagnostics, Salmaan
Karim alisema JKCI ni miongoni mwa taasisi chache wanazofanya nazo kazi kwa
urahisi na ushirikiano mzuri ikilinganishwaa taasisi nyingine.
Meneja Msaidizi wa Mauzo kutoka Cardimed Africa L.t.d, Linda Tegambwage alisema kikao hicho kimeimarisha uelewa na mahusiano kati ya wazabuni na uongozi wa JKCI, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wazi na mawasiliano ya mara kwa mara ni msingi wa kuhakikisha vifaa tiba na huduma zinapatikana kwa wakati na kwa ubora unaokidhi mahitaji ya wagonjwa.
Comments
Post a Comment