JKCI yaiweka Tanzania kileleni Afrika Mashariki na Kati kwa upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu za moyo bila kufungua kifua (TAVI)


Wataalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka nchini India wakifanya upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo kwa njia ya tundu dogo bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation - TAVI) katika kambi maalumu ya siku moja ambapo wagonjwa wawili walifanyiwa upasuaji.

Wataalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka nchini India wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo kwa njia ya tundu dogo bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation - TAVI) katika kambi maalumu ya siku moja ambapo wagonjwa wawili walifanyiwa upasuaji.

 Wataalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka nchini India wakiangalia upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo kwa njia ya tundu dogo ulivyofanyika bila ya kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation - TAVI) katika kambi maalumu ya siku moja ambapo wagonjwa wawili walifanyiwa upasuaji.

**************************************************************************************************************************************************************************************************

Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane amesema Taasisi hiyo imeendelea kuimarisha huduma za kibingwa kwa kufanya upasuaji wa kisasa wa kubadilisha valvu ya moyo bila kufungua kifua, hatua iliyookoa zaidi ya shilingi milioni 200 kwa wagonjwa waliofanyiwa matibabu hayo.

Dkt. Waane alisema upasuaji huo uliofanyika jana unajulikana kitaalamu kama Transcatheter Aortic Valve Implantation (TAVI) hufanyika katika Taasisi chache sana Afrika Mashariki na Kati, huku Tanzania ikiwa nchi pekee inayotoa huduma hiyo kwa sasa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

“Upasuaji huu unafanyika kwa wagonjwa ambao hawawezi kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, hususan wazee au wenye magonjwa mengine sugu. Tunafanya kwa kufungua tundu dogo badala ya kupasua kifua hivyo hupunguza hatari, maumivu na muda wa kupona,” alisema Dkt. Waane.

Alieleza kuwa katika kambi maalumu ya matibabu hayo ya siku moja, JKCI imewafanyia upasuaji wagonjwa wawili, ikiwa ni mara ya tatu kufanyika kwa aina hiyo ya upasuaji huku jumla ya wagonjwa tisa wakinufaika kupitia kambi tofauti tofauti.

Kwa mujibu wa Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba alisema gharama ya upasuaji huo ni kubwa kutokana na matumizi ya vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi, ikiwemo India na Marekani, ambapo gharama ya mgonjwa mmoja kutibiwa nje ya nchi hufikia kati ya shilingi milioni 50 hadi 90.

“Hapa nchini, serikali inachangia kati ya asilimia 80 hadi 90 ya gharama za matibabu haya kupitia mfuko wa tiba bobezi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma hizi bila kusafiri nje ya nchi,” aliongeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Moyo kwa watu wazima wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo  Dkt. George Longopa alisema faida kubwa ya upasuaji huo ni mgonjwa kutopata kovu kifuani pamoja na kuimarika kwa ufanisi wa valvu mpya inayowekwa.

“Hapo awali kwa wagonjwa wa aina hii tulikuwa tukifanya upasuaji wa kufungua kifua, lakini sasa tunafanya bila kufungua kifua. Hii ni kambi ya tatu na tayari wataalamu wetu wa ndani wamejijengea uwezo wa kuufanya upasuaji huu wenyewe,” alisema Dkt. Longopa ambaye pia ni mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

Alifafanua kuwa wagonjwa waliopatiwa huduma hiyo ni wale waliokuwa na tatizo la kuziba kwa valvu ya kusukuma damu kutoka moyoni, hivyo kuondolewa valvu iliyoharibika na kuwekwa valvu bandia kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Katika kambi hiyo, JKCI ilishirikiana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka India, Nilay Patel ambaye alisema teknolojia ya matibabu hayo inalenga zaidi wagonjwa wenye umri mkubwa ili kupunguza madhara ya kiafya yanayoweza kujitokeza.

“Nimefurahishwa sana na ubora wa wataalamu wa JKCI pamoja na vifaa vya kisasa walivyonavyo. Hii ni Taasisi ya mfano Afrika Mashariki,” alisema Dkt. Patel ambaye pia ni mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Cardimed Africa, Nelly Otenyo alisema kampuni yake imeendelea kushirikiana na JKCI tangu mwaka 2017 katika kusambaza vifaa tiba vinavyotumika kwenye upasuaji huo wa TAVI.

“Tunaona fahari kuona madaktari wa ndani sasa wana uwezo wa kufanya upasuaji huu hapa nchini. Zamani wagonjwa walilazimika kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa, lakini sasa huduma hizi zinapatikana ndani ya Tanzania,” alisema Otenyo.

Upasuaji wa TAVI unatajwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wagonjwa wa moyo, hususan wazee, na ni ushahidi wa uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali katika kuboresha huduma za afya za kibingwa nchini.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo