Wafanyakazi wa MSD wafundishwa njia madhubuti za kujikinga na magonjwa ya moyo.
Mtaalamu
wa tiba viungo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar
Group Jackline Mariki akitoa elimu kuhusu afya bora mahala pa kazi wakati wa
kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa Boharai Kuu
ya Dawa (MSD) iliyoanza leo katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Mboyi Wishega
akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wafanyakazi wa MSD wakati wa kambi maalumu
ya siku mbili ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu kutoka Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed
Aloyce akimuonesha namna uwiano wa uzito na urefu unavyatakiwa kuwa Mfanyakazi
wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Christopher Komba wakati wa
kambi maalumu ya siku mbili ya uchunguzi wa afya inayofanywa na wataalamu
kutoka JKCI katika ofisi za MSD zilizopo jijini Dar es Salaam.
Picha
na Khamis Mussa
***********************************************************************************************************
Wafanyakazi
wanaotumia muda mwingi maofisini wametakiwa kujenga utamaduni wa kufanya
uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
yakiwemo shinikizo la juu la damu na magonjwa ya moyo.
Hayo
yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Daktari
bingwa wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophilly Mushi wakati akitoa mafunzo maalumu kuhusu namna
ya kuzuia magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu katika kambi maalumu ya
siku mbili ya upimaji wa afya kwa wafanyakazi wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Akizungumzia
hali ya afya nchini, Dkt. Theophilly alisema takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha
kuwa asilimia 20 ya vijana nchini wanakabiliwa na ugonjwa wa shinikizo la juu
la damu, huku upande wa watu wazima tatizo hilo likichukua asilimia 35%.
“Mazingira
ya kazi za mijini, kushindwa kupata nafasi ya kufika katika vituo vya afya ili
kufanya uchunguzi wa afya, kazi za kukaa muda mrefu ofisini bila mazoezi, vimechangia
kwa kiasi kikubwa ongezeko la magonjwa ya moyo miongoni mwa wafanyakazi
wanaotumia muda mwingi ofisini”, alisema Dkt. Theophilly
“Magonjwa
ya moyo na shikinizo la juu la damu yameendelea kuwa tishio kubwa kwa jamii
hususani wafanyakazi wa mijini ndio maana leo tumefika MSD ili kutoa elimu ya
afya bora mahali pa kazi, kufanya upimaji wa afya, kuwapa elumu kuhusu umuhimu
wa kufanya mazoezi, kuzingatia uzito wenu wa mwili na kuzingatia lishe bora,”
alisema Dkt. Theophilly.
Kwa
upande wake Mtaalamu wa tiba viungo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Hospitali ya Dar Group Jackline Mariki alisema ni muhimu wafanyakazi
wakazingatia afya mahali pa kazi ili kuepuka maumivu ya shingo mabega na mgongo
yanayotokana na kukaa kwa muda mrefu na kutokukaa kama inavyotakiwa.
“Tumeona ni muhimu tukawaelimisha wafanyakazi
kuhusu afya mahali pa kazi ili waweze kufahamu namna sahihi ya kukaa, aina ya
viti vitakavyowaepusha kupata shida za mgongo, namna nzuri ya kunyanyua vitu na
kupanga vifaa ili waweze kujikinga na magonjwa ya viungo vya mwili,” alisema
Jackline.
Nao
wafanyakazi wa MSD walisema mafunzo waliyoyapata yamewapa uelewa mpana kuhusu
umuhimu wa kujali afya zao hivyo kuepuka kupata maradhi yanayoweza kuzuilika
endapo hatua za kinga zitazingatiwa ipasavyo.
“Nawashukuru sana wataalamu wa JKCI kwa kutufiika
na kutupa elimu ambayo itanisaidia kujikinga na magonjwa ya moyo, kinga ni bora
kuliko tiba nitatumia elimu niliyoipata kufanya mazoezi yatakayoniepusha na
magonjwa hayo,” alisema Emanuel Kiunga, Afisa Tehama Mwandamizi kutoka Bohari Kuu
ya Dawa (MSD).
“Kama mfanyakazi ninayetumia muda mwingi kukaa
ofisini nimejifunza kupangilia muda wangu ili niweze kupata na muda wa
kuchunguza afya yangu na kujilinda na magonjwa yasiyoambukiza, pia nitazingatia
ushauri tuliopewa na wataalamu ili afya yangu iwe imara wakati wote,” alisema
Dorothy Mtatifikolo.





Comments
Post a Comment