Mchengerwa asema JKCI nguzo huduma za afya AFCON

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi kitabu Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kinachohusu watoto waliozaliwa kabla ya muda (watoto njiti) alipotembelea hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) katika ziara yake ya kuangalia  maandalizi ya kitiba kuelekea mashindano ya  AFCON 2027 aliyoifanya katika hospitali hiyo.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akipokea ua kutoka kwa Victoria Komba alipotembelea hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwa sasa inasimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni  maandalizi ya kitiba kuelekea mashindano ya  AFCON 2027.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Salehe Mwinchete akimueleza Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa kuhusu vifaa vya kisasa vinavyosaidia kuwatunza watoto waliozaliwa kabla ya muda (watoto njiti) katika ziara yake ya kuangalia  maandalizi ya kitiba kuelekea mashindano ya  AFCON 2027 aliyoifanya katika hospitali hiyo.

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akipanda mti katika Hospital ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Mhe. Mchengerwa alipanda mti huo alipotembelea hospitali hiyo kwaajili ya ziara ya kuangalia maandalizi ya kitiba kueleka AFCON 2027.


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mhe. Amos Makalla, akipanda mti katika Hospital ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ikiwa ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. 

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na wafanyakazi wa afya na wananchi wa Arusha alipotembelea hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa  na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika ziara yake ya kuangalia  ikiwa ni  maandalizi ya kitiba kuelekea mashindano ya  AFCON 2027.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge  akisoma taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa alipotembelea hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayo kwasasa inasimamiwa na JKCI, kwaajili ya kuangalia maandalizi ya kitiba kuelekea mashindano ya  AFCON 2027.

***********************************************************************************************************************************************************************************************

Tanzania iko tayari kutoa huduma za afya za kibingwa na kibobezi kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya nchi katika kuimarisha maandalizi ya kitabibu kuelekea Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, leo jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kutembelea ALMC ambayo hivi sasa inasimamiwa na JKCI ikiwa ni maandalizi ya kitabibu kuelekea AFCON 2027.

Mhe. Waziri Mchengerwa alisema zaidi ya kuwa tukio la michezo, AFCON 2027 pia itakuwa ni fursa adhimu ya kimkakati kwa Tanzania kujitangaza kimataifa katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, afya na uwekezaji.

“Hivi sasa tunajiandaa na michuano ya AFCON, kupitia maandalizi haya, serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya, kuimarisha uwezo wa wataalamu wa tiba na kuhakikisha uwepo wa huduma za dharura za kiwango cha juu zitakazokidhi mahitaji ya wachezaji, wageni na wananchi kwa ujumla,”alisema Mhe. Waziri Mchengerwa.

Alibainisha kuwa ushirikiano kati ya taasisi hizo kupitia Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ni wa kimkakati, wenye tija kwa sasa na wenye manufaa makubwa kwa mustakabali wa sekta ya afya nchini.

Akizungumza kuhusu changamoto ya magonjwa yasiyoambukiza, Mhe. Waziri Mchengerwa alinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazoonesha kuwa zaidi ya vifo milioni 17.5 duniani, sawa na asilimia 32 husababishwa na magonjwa ya moyo, huku Mkoa wa Arusha ukiwa ni  miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya wagonjwa wa magonjwa hayo.

Alitoa wito kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote huku akisisitiza kuwa ni kinga muhimu ya kifedha na nyenzo ya kuokoa maisha wakati ambapo hauna fedha za matibabu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Makalla, alisema mkoa huo umejipanga kikamilifu katika maandalizi ya kitabibu kuelekea AFCON 2027, huku akibainisha kuwa JKCI iko tayari kutoa huduma za matibabu ya moyo kwa wananchi pamoja na wageni watakaohudhuria michuano hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dk. Peter Kisenge, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Alisema taasisi hiyo tayari imewahudumia zaidi ya wagonjwa 26,000 kupitia huduma ya tiba mkoba na ina matawi saba nchini.

Dk. Kisenge aliongeza kuwa JKCI imeanza kutumia teknolojia ya akiliunde (Artificial Intelligence – AI) pamoja na mifumo ya kidijitali kufuatilia maendeleo ya wagonjwa baada ya matibabu, sambamba na kufanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na upasuaji wa kisasa wa matundu madogo.

“Tupo katika mpango wa kuanzisha maabara kubwa yenye vifaa vya kisasa ikiwemo MRI na CT Scan. Tayari mwekezaji kutoka China ameonesha nia ya kuwekeza katika hospitali hii,” alisema.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mtaalamu wa kupandikiza vifaa visaidizi vya moyo alisema JKCI imepokea maombi ya ushirikiano kutoka nchi za Kongo na Burkina Faso katika huduma za magonjwa ya moyo na tiba utalii, hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya serikali na kuiweka Tanzania katika ramani ya huduma za afya za kibingwa barani Afrika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe alisema ushirikiano kati ya serikali, taasisi za dini na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanafanikiwa kwa viwango vya juu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya ALMC, Peter Maduki alisema ushirikiano kati ya JKCI na Dayosisi ya Kaskazini Kati ya KKKT ni wa kipekee na umechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo