JKCI kuanza mchakato wa upandikizaji wa moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akimkabidhi mfano wa moyo Mwenyekiti wa kamati ya
upandikizaji wa moyo Dkt. Everist Nyawawa wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo leo
katika ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)
Dkt. Peter Kisenge akiwajulia hali wanachama wa chama cha wagonjwa wa moyo nchini wakati wa uzinduzi wa kamati ya upandikizaji wa moyo uliofanyika leo
katika ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wanachama wa chama cha wagonjwa wa moyo nchini wakisikiliza wakati wa uzinduzi wa kamati ya upandikizaji wa moyo uliofanyika leo katika ukumbi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) uliopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI
*************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza mchakato wa
kuanzisha huduma ya upandikizaji wa moyo inayotarajiwa kukamilika baada ya
miaka mitano na kuanza kutoa huduma hiyo.
Kukamilika kwa mchakato huo kunatarajiwa kuendelea kuiweka
Tanzania kwenye ramani ya nchi inayotoa huduma za juu za matibabu ya moyo
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi
Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge alisema mchakato huo ni wakihistoria na
utafungua ukurasa mpya katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo nchini.
Dkt. Kisenge alisema katika kuelekea maadhimisho ya Miaka 10
ya JKCI taasisi hiyo imeona ianze kuweka mikakati ya kutoa huduma ya
kupandikiza moyo kwani ni huduma ambayo imekuwa ikitafutwa na wagonjwa wengi wa
moyo katika bara la Afrika.
"Tayari tumezindua Kamati maalum ya upandikizaji wa moyo
itakayosimamia maandalizi yote ya kitaalamu, kisheria na kiutendaji ndani ya
kipindi cha miaka mitano. Hii ni hatua kubwa kwa nchi yetu na pia kwa nchi
jirani ambazo hazina huduma hii," alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema huduma hiyo ya upandikizaji wa moyo ina
mchakato wa muda mrefu na maandalizi yakutosha katika maeneo mbalimbali ikiwemo
uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa, mafunzo ya wataalamu, pamoja na utaratibu
wa kisheria na kimaadili.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Upandikizaji wa Moyo
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Evarist Nyawawa alisema utekelezaji
wa mpango huo utafuata mifumo bora ya utoaji wa huduma hiyo kukidhi viwango vya
kimataifa.
Dkt. Nyawawa ambaye pia ni bingwa wa upasuaji wa moyo katika
Taasisi hiyo alisema takwimu zinaonesha watu zaidi ya 50,000 duniani wameshafanyiwa
upandikizaji wa moyo na umekuwa wa mafanikio hivyo hata JKCI itaweza kutoa
huduma hiyo.
Mpango huo ni sehemu ya jitihada za JKCI katika kuimarisha
huduma za kitaifa na kimataifa za moyo kupunguza rufaa za nje ya nchi na
kuifanya taasisi hiyo kuwa kitovu cha huduma za moyo ukanda ya Afrika Mashariki
na kati.
Comments
Post a Comment