Watu 537 wapimwa moyo Arusha kambi ya madaktari bingwa wabobezi
Daktari bingwa wa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rose Chengo akimpima mapigo ya moyo mtoto aliyeletwa na mzazi wake kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyomalizika hivi karibuni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Amad Mlilapi akimpima shinikizo la damu mkazi wa Arusha wakati wa kambi maalum ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyomalizika hivi karibuni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Bertha Massawe akimsomea majibu ya mfumo wa umeme wa moyo mwananchi aliyefika kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyomalizika hivi karibuni katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
********************************************************************************************************************************************************************************************
Watu 537 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu ya moyo bila malipo katika kambi maalum ya madaktari bingwa na wabobezi wa magonjwa mbalimbali iliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mohamed Aloyce wakati wa kuhitimisha huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi hiyo.
Dkt. Aloyce alisema kati ya watu waliopimwa 503 walikuwa ni watu wazima na watoto 34 ambapo wanawake walikuwa 366 na wanaume 171.
“Kati ya watu wote tuliowapima watu 376 ambao ni sawa na asilimia 70 walikutwa wakiwa na afya nzuri ya moyo huku 161 sawa na asilimia 30 walibainika kuwa na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwemo mfumo wa umeme wa moyo, valvu, mishipa ya damu ya moyo na moyo kutanuka”.
“Takwimu hizi zinaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo mara kwa mara kwa wananchi ambao walikuwa hawafikiwi na huduma hii ya kibingwa”.
“Katika kambi hiyo wagonjwa 24 walikutwa na matatizo yaliyohitaji uchunguzi zaidi pamoja na kupata matibabu ya kibingwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo Upanga jijini Dar es Salaam wagonjwa hawa watu wazima 15 na watoto 9 tumewapa rufaa”, alisema Dkt. Aloyce.
Kwa upande wake daktari bingwa wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Rose Chengo alisema baadhi ya watoto waliopimwa walikuwa wakikabiliwa na dalili kama kuchelewa kukuwa, kupungua uzito au kushindwa kushiriki shughuli za kawaida kulingana na umri wao.
Comments
Post a Comment