Wanaume wajitokeza kwa wingi kupima moyo Sabasaba

Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Victoria Ngalomba akimpima wingi wa sukari kwenye damu mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo lililopo katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.


Daktari wa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ahmed Mchina akisikiliza mapigo ya moyo ya mtoto aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerete barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

**********************************************************************************************************************************************************************************************

Watu 755 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo kwenye Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elius Birago alisema kati ya watu waliowaona kwa muda wa siku saba wanaume walikuwa wengi zaidi ukilinganisha na wanawake.

Dkt. Birago alisema wanaume waliowaona walikuwa 415, wanawake 319 na watoto 21 huku wengi wao wakiwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kisukari na kuna ambao hawakujijua kabisa kuwa na tatizo hilo lakini baada ya kupata vipimo wamekutwa na shida.

“Katika maonesho ya mwaka huu wanaume wamejitokeza kwa wingi zaidi kupima afya zao ukilinganisha na mwaka jana ambapo wanawake walikuwa wengi zaidi, maonesho haya yamekuwa na faida kwao kwani wamepewa ushauri na wengine wamepata rufaa kwa ajili ya kuanza kliniki”, alisema Dkt.Birago.

“Kuna ambao walikuwa wanapita njia baada ya kuona tuko hapa wakaja kupima afya za mioyo yao, kuna ambao tumewakuta na dalili za saratani tumewaelekeza waende banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road na wengine tuliowakuta na  dalili za magonjwa mengine tumewaelekeza waende katika banda la Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dkt. Birago aliwaomba wananchi watumie maonesho hayo kupima afya zao pia wawe na tabia ya kupima afya ya moyo mara kwa mara kwani ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hauna dalili na wengine wanapata dalili wakati tayari wameshapata madhara ya ugonjwa huo.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua hali za mioyo yao na kuokoa muda wa kuifuata huduma hiyo hospitali.

“Nilisikia katika vyombo vya habari kuwa huduma za upimaji wa moyo zinatolewa katika banda hili nami nikaona nije kupima ingawa nilikuwa na hofu ya kutumia muda mwingi kusubiri kupata huduma lakini nimetumia muda mfupi kupima na nimeandikiwa dawa za kutumia”, alisema Jackson Urio mkazi wa Kigamboni.

“Ni mara yangu ya kwanza kupima vipimo vya moyo, leo nimepima na wamenikuta mfumo wangu wa umeme wa  moyo uko chini nimepewa rufaa ya kwenda JKCI kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi na kupewa huduma ya haraka”.

“Ninawasihi wananchi wenzangu wanaokuja katika maonesho ya Sabasaba watumie nafasi hii kupima afya zao kwani huduma hii inapatikana hapa na ni nzuri, watoa huduma wamejipanga pia hakuna foleni”, alisema Asha Juma mkazi wa Bagamoyo.


Comments

Popular posts from this blog

JKCI na AICC Hospitali kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kikao kazi cha wenyeviti na watendaji wakuu wa Taasisi za Umma

JKCI yapata tuzo ya taasisi ambayo imetoa mchango wa kipekee kiuchumi na kijamii katika kuleta matokeo makubwa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024

Wafanyakazi waliohama JKCI waagwa