JKCI kutumia akiliunde kumtambua mtu kama atakuwa na magonjwa ya moyo baada ya miaka 10 ijayo
Mkurugenzi wa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Robert Mallya akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani Dkt. Jasjit Suri alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona namna watakavyotumia akiliunde kufanya uchunguzi utakaotambua hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo.
Mkuu wa Kitengo cha Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Thadeo Kavishe akimweleza Mkurugenzi wa Kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani Dkt. Jasjit Suri vipimo vinavyofanyika katika maabara hiyo wakati Mkurugenzi huyo alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona namna watakavyotumia akiliunde kufanya uchunguzi utakaotambua hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo.
Mkuu wa Kitengo cha Radiolojia wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Praygod Lekasio akimweleza Mkurugenzi wa Kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani Dkt. Jasjit Suri jinsi huduma za radiolojia zinavyotolewa kwa wagonjwa wakati Mkurugenzi huyo alipotembelea taasisi hiyo jana kwaajili ya kuona namna watakavyotumia akiliunde kufanya uchunguzi utakaotambua hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo.
***************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na Kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani kutumia akiliunde katika kufanya uchunguzi ambao utatambua hatari ya mtu kupata magonjwa ya moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa
Upasuaji wa Taasisi hiyo Dkt. Angela Muhozya wakati akiongea na waandishi wa
habari kuhusu ushirikiano unaokwenda kufanyika kati ya JKCI na kampuni hiyo.
Dkt. Angela alisema kupitia akiliunde
wataweza kuzuia mtu kupata magonjwa ya moyo kwa kufanya vipimo vya moyo na
mishipa ya damu na kutoa ushauri wa
jinsi gani mtu anaweza kubadili mtindo wa maisha kwa kula vyakula bora, kufanya
mazoezi, kutumia dawa stahiki kwa wale wenye magonjwa ya moyo tayari, kutokunywa
pombe kupitiliza na kuacha kutumia bidhaa bidhaa hatarishi kwa mioyo yao kama tumbaku ambazo zinaathari kubwa kiafya.
‘’Teknologia hii ya akiliunde iliyojikita
katika kuzuia magonjwa ya moyo ambayo itaanza kutumika katika taasisi yetu itatusaidia
kuwafikia watanzania wengi zaidi kwa kufanya uchunguzi na kutambua magonjwa ya moyo
miaka 10 kabla ya mtu kupata tatizo”, alisema Dkt Angela.
Dkt. Angela aliwaomba wananchi kufika
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili waweze kukutana na teknologia hiyo iliyojikita
zaidi katika kuzuia magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa kuwa wanaamini kinga ni bora zaidi kuliko tiba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara
ya Radiolojia kutoka Wizara ya Afya Gelard
Mrema alisema ushirikiano unaokwenda kufanyika baina ya JKCI na kampuni ya AtheroPoint inayotumia akiliunde kutambua
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu utawasaidia watanzania wengi kufahamu hali
za mioyo yao zitakavyokuwa miaka 10 ijayo.
“Sisi kama Wizara tumeona tija ya kuleta
kampuni ya AtheroPoint kwenye Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete kwani
wanateknlolojia ambayo itaweza kumchunguza mgonjwa atakuwa na shida gani ya
moyo na mishipa ya damu baada ya miaka 10 ijayo, huduma hii itapatikana JKCI siku chache zijazo”,
alisema Mrema.
Naye Mkurugenzi kutoka kampuni ya AtheroPoint ya nchini Marekani Dkt.
Jasjit Suri alishukuru kupata fursa ya kutoa elimu ya matumizi ya akiliunde katika
kutambua magonjwa ya moyo katika miaka 10 ijayo na kuahidi kushirikiana na
taasisi hiyo ili waweze kufikia maono yao ya kutoa huduma bora na za kisasa za
matibabu ya moyo na mishipa ya damu.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inazidi kuimarisha utoaji wa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo nchini lengo likiwa ni watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi wafikiwe na huduma za ubingwa bobezi za matibabu ya moyo.
Comments
Post a Comment