JKCI yatoa elimu ya lishe kwa kutumia pyramid ya vyakula halisi
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akiwafundisha watoto waliotembelea banda la Taasisi hiyo makundi ya vyakula na aina ya vyakula hivyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Hospitali ya Dar Group France Kapele akiwafundisha wanafunzi kutoka
shule ya Maximilian namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa dharura
walipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu
Nyerete barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
********************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Wananchi wanaotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) lililopo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam wanapata elimu ya lishe bora inayotolewa kwa vitendo kwa kutumia shelfu “pyramid” yenye vyakula halisi kuelezea makundi ya vyakula, umuhimu wake na namna ya kuvitumia.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mtaalamu wa Lishe wa taasisi hiyo Husna Faraji alisema elimu ya lishe ni muhimu kwani inatoa matibabu kwa watu mwenye changamoto za magonjwa ya moyo ambao mara nyingi wanapaswa kufuata ushauri wa mtaalamu wa lishe katika kuandaa vyakula wanavyotumia.
Husna alisena wapo kwenye maonesho ya Sabasaba wanatoa ushauri wa lishe bora, kwani matumizi ya chakula yanapaswa kuendana na hali ya kiafya ya mtu, jukumu lao ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ndio maana wamewaletea shelfu hilo lenye vyakula halisi ili waweze kujifunza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliopata huduma hiyo walisema watanzania wengi wamekuwa wakitumia vyakula bila kuchanganya makundi yote ya vyakula kwani wengi wamekuwa wakila chakula ili washibe.
Eustack Moshi mkazi wa Dar es Salaam alisema kutokana na elimu ya lishe waliyoipata amegundua kuwa baadhi ya vyakula anavyotumia kwa wingi havina umuhimu katika mwili wake bali vinaweza kumsababishia kupata magonjwa yasiyoambukiza.
“Nimekuwa nikila vyakula vyenye mafuta mengi bila kujua madhara yake kwani Afisa lishe kanifundisha kuwa mafuta mengi yanaweza kusababisha kuziba kwa mishipa yangu ya damu na kuniletea shida za moyo, Sasa nimeelimika na nitaanza kubadilisha mfumo wangu wa maisha katika masuala ya lishe,” alisema Eustack.
Naye Zainabu Hassani alisema amepata ushauri wa lishe bora katika Taasisi hiyo utakayomsaidia kupunguza uzito wake ili urefu wake uweze kuendana na uzito wake kwa kuzingatia lishe bora.
“Mtaalamu wa lishe amenishauri nile zaidi matunda na mboga za majani huku nikipunguza wanga na mafuta mengi kuweka sawa uzito wangu,” alisema Zainabu.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inaendelea kutoa huduma mbalimbali za uchunguzi na matibabu ya moyo katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) wakiwa na kauli mbiu ya Afya ya Moyo Wako ni Jukumu Lao.
Comments
Post a Comment