JKCI yaihamasisha jamii kupata chanjo ya homa ya ini
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Florah
Kasembe akitoa elimu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo kwa wananchi
waliotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya 49 ya Biashara ya
Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA).
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Kajangwa akimpima wingi wa sukari kwenye damu mwananchi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Mhasibu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) DianaRose
Kaugila akizungumza na mwananchi aliyefika katika banda la Taasisi hiyo
kwaajili ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 49 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja
vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI
*******************************************************************************************************
Jamii imehamasishwa kujitokeza kufanya kipimo na kupata chanjo
ya ugonjwa wa homa ya ini ambao umekuwa tatizo kubwa katika jamii kwani virusi vya
homa hiyo vipo na vinaambukiza kwa kasi.
Rai hiyo imetolewa leo na Daktari wa usalama mahala pa kazi
kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias
Birago wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
(SABASABA).
Dkt. Birago alisema virusi vya homa hiyo vinaambukiza kwa
njia ya majimaji yanayotoka katika mwili wa binadamu mwenye maambukizi ikiwemo
damu, jasho, maji ya uzazi “Amniotic
fluid”, kujamiiana pamoja na matumizi ya vifaa vyenye ncha kali
vilivyotumika kwa mgonjwa wa homa ya ini.
“Lengo letu kubwa kutoa huduma hii katika maonesho ya
Sabasaba ni kuikinga jamii isipate maambukizi ya homa ya ini, wale tutakaowapima
na kuwakuta na shida tutawaelekeza namna nzuri ya kupata matibabu na kwa wale
ambao wako salama watapata chanjo kupitia maonesho haya”, alisema Dkt. Birago
Dkt. Birago alisema dalili za awali za ugonjwa huo zinaweza zisionekane
lakini ugonjwa unavyoendelea mtu anaweza kupata manjano, mwili kuchoka, ngozi
kuwasha, kupata homa, kupungua uzito hivyo kupeleka ini kushindwa kufanya kazi.
“Tumeweza kutoa elimu na umuhimu wa kujikinga na ugonjwa wa
homa ya ini kwa jamii kupitia maonesho haya kuiwezesha jamii kujua tatizo hilo
kuwa lipo na halina dawa lakini lina kinga iwapo mtu atafanya kipimo na kupata
chanjo yake”, alisema Dkt. Birago
Dkt. Birago alisema JKCI kupitia kitengo cha Usalama mahala
pa kazi kilichopo Hospitali ya Dar Group wamekuwa wakitembelea taasisi na
mashirika mbalimbali kwaajili ya kutoa elimu ya namna ya kujikinga na ugonjwa
wa homa ya ini.
Kwa upande wake Afisa Uuguzi wa Taasisi hiyo Florah Kasema
alisema wananchi waliotembelea banda la JKCI wamehamasika kupata chanjo hiyo
ambayo wengi wao hawakuwa wakifahamu madhara yake.
Florah alisema ugonjwa wa homa ya ini unaongezeka kwa kasi na
kuathiri jamii hivyo wataalamu wa JKCI hawataishia kutoa huduma hiyo katika
maonesho ya Sabasaba bali wataendelea kutoa elimu na chanjo hiyo katika vituo
vyao vya afya.
“Ni muhimu wale wote walioanza kupata chanjo ya homa ya ini
kuhakikisha wanamaliza chanjo hiyo kwa kupata chanjo zote tatu kwa kipindi cha
miezi sita kama ambavyo wameshauriwa na wataalamu wa afya”, alisema Florah
Comments
Post a Comment