Watu 1,369 wafanyiwa uchunguzi wa moyo maonesho ya Sabasaba
Afisa Uuguzi kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group France Kapele akimfundisha mwananchi namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mgonjwa wa dharura alipotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika viwanja vya Mwalimu Nyerete barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Mjumbe wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Irene Mbonde akizungumza na wananchi waliofika katika banda la taasisi hiyo kwaajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho Sabasaba yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
***************************************************************************************************************************************************************************************
Watu 1,369 wakiwemo watu wazima 1,289 na watoto 80 wamepata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa maonesho ya Sabasaba yaliyomalizika hivi karibuni.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo
cha Uhusiano na Mawasiliano wa Taasisi hiyo Anna Nkinda wakati akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu huduma walizozitoa katika maonesho hayo.
Anna alisema baada ya kufanyiwa vipimo vya moyo na kupata
matibabu, watu 217 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo ikiwa
ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kina zaidi ambapo watu wazima walikuwa 209 na watoto 8.
“Watu 371 walifanyiwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo
unavyofanya kazi na watu 336 walifanyiwa kipimo cha kuangalia mfumo wa umeme wa
moyo, vipimo vya maabara vilifanyika kwa watu 763 ambao walichunguzwa matatizo
ya figo, ini, kiwango cha mafuta mwilini, pamoja na homa ya ini”.
“Watu 145 walipata elimu ya mtu mmoja mmoja ya ushauri wa lishe
na kufuata mtindo bora wa maisha kutoka kwa mtaalamu wetu wa lishe ambao
utawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo”,
alisema Anna.
Anna aliwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya za
mioyo yao hasa pale ambapo taasisi hiyo inakuwa ikitoa huduma za upimaji na matibabu ya moyo kwa
wananchi kwa kuwafuata mahali walipo katika program yake ijulikanayo kwa jina
la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma katika banda hilo walishukuru kwa
huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kujua afya za mioyo yao zikoje.
“Sijawahi kupimwa moyo katika maisha yangu, baada ya kusikia
huduma ya upimaji inapatikana katika maonesho ya Sabasaba niliona nami nije kupima, nashukuru sana moyo
wangu uko salama. Nimepewa ushauri wa jinsi ya kuutunza ili usipate madhara
siku za mbeleni”, alishukuru Amon Mwasote mkazi wa Mkuranga.
“Mwanangu alikuwa na tatizo la kutokukua vizuri na kuchoka
haraka anapocheza na wenzake, nilimpeleka katika hospitali kadhaa kutibiwa
lakini hakupona, baada ya kufanyiwa vipimo amekutwa na tatizo la tundu kwenye
moyo. Amepewa rufaa ya kwenda kutibiwa
JKCI”, alisema Jemima Masanja mkazi wa Morogoro.
Katika maonesho hayo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ilishika nafasi ya mshindi wa pili katika kundi la watoa huduma za afya.
Comments
Post a Comment