Tanzania yashiriki maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia
Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule akipokea zawadi ya picha ya moyo kutoka kwa Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph alipotembelea banda la taasisi hiyo leo katika maonesho ya 97ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka. Kushoto ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi hiyo Amanda Anyoti.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Joseph akizungumza na mkazi wa Zambia aliyefika katika banda la taasisi hiyo leo kwaajili ya kupata ushauri wa matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia yanayofanyika jijini Lusaka.
**************************************************************************************************************************************************************************************************
Tanzania inashiriki katika maonesho ya 97 ya Kilimo na Biashara ya Zambia ikiwa na lengo la kutangaza huduma za matibabu ya ubingwa bobezi zinazopatikana nchini pamoja na huduma za usafirishaji.
Hayo yamesemwa leo na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Generali Mathew Edward Mkingule wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu nchi hiyo kushiriki katika
maonesho hayo yanayofanyika jijini Lusaka.
Alisema kwa mara ya kwanza Taasisi kubwa tano zinazotoa
huduma za afya na usafirishaji zimeshiriki katika maonesho hayo na hivyo
Tanzania kupata nafasi ya kutangaza huduma inazozitoa kwa wananchi wa Zambia na
washiriki wa maonesho hayo.
“Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia umeratibu ushiriki wa taasisi
zetu kubwa tano katika maonesho haya ambazo ni Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa
ya Kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na
Shirika la Ndege la Air Tanzania”.
“Serikali yetu imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya
ikiwemo kujenga majengo ya kisasa, kununua vifaa tiba vya kisasa na kusomesha wataalamu
katika ngazi ya ubingwa bobezi, kushiriki kwa taasisi hizi katika maonesho haya
kutawawezesha kutangaza huduma wanazozitoa na wagonjwa wengi kuja kutibiwa
katika nchi yetu na kutuingizia fedha za
kigeni’, alisema Mhe. Balozi Luteni Generali Mkingule.
Alisema wafanyabiasha wengi wa Zambia wanakuja nchini kununua
bidhaa na wengine wanakwenda nje ya nchi imefika wakati sasa kwa
wafanyabiashara hao kutumia bandari ya Dar es Salaam ambayo ni lango kuu la
biashara katika nchi wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kusafirisha
mizigo yao na wasafiri kwa kutumia Shirika
la ndege la Air Tanzania ambalo ndege
zake zinakwenda katika nchi za SADC.
Kwa upande wa washiriki wa maonesho hayo walishukuru kwa
kupata nafasi ya kushiriki katika maonesho hayo na kusema kuwa wamejipanga
kutangaza huduma zinazotolewa katika taasisi zao ili wananchi wa Zambia na
mataifa mengine yanayoshiriki katika maonesho hayo waende Tanzania kufuata
huduma hizo pia watumie huduma hizo pale watakaposafiri au kusafirisha mizigo
yao.
“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) inashiriki katika
maonesho ya 79 ya Kilimo na Biashara ya Zambia kwa kutangaza huduma za matibabu
ya moyo tunazozitoa, kutoa elimu ya magonjwa ya moyo na kutoa ushauri wa
kitaalamu kwa watu wenye matatizo ya moyo”.
“Taasisi yetu ni moja ya taasisi bora barani Afrika inayotoa
huduma za ubingwa bobezi wa matibabu ya moyo, tumejipanga kuwafikia wagonjwa
wengi zaidi ndani na nje ya nchi na ndiyo maana tuko hapa kutangaza huduma ya
utalii wa matibabu ambayo inapatikana nchini kwetu”, alisema Dkt. Alex Joseph
ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu.
“Tunafurahi kushiriki katika maonesho haya ya 97 ya Kilimo na
Biashara hapa Zambia, tunatumia nafasi hii kutoa ushauri wa kibingwa bobezi kwa
wananchi wa Zambia na washiriki wote wa maonyesho haya na kutangaza kliniki yetu
ya wagonjwa maalumu (VIP) na wa Kimataifa inayopatikana katika Taasisi yetu ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI)”,
alisema Daktari bingwa wa mifupa Joseph Lamtane.
“Hospitali ya Rufaa ya
Kanda Mbeya (MZRH) inashiriki katika maonesho haya kwa kutangaza huduma za matibabu
ya ubingwa bobezi tunazozitoa katika hospitali yetu huduma hizo ni pamoja na matibabu
ya saratani, kwa kuwa Mbeya ni karibu na Zambia ninaamini baanda ya maonesho
haya wagonjwa wengi kutoka Zambia watakuja kutibiwa”, alisema Daktari bingwa wa
upasuaji kwa watoto Lazaro Mboma.


Comments
Post a Comment