Wananchi wahimizwa kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya mo
Mjumbe wa Taasisi isiyo
ya Kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) Irene Mbonde akiwakabidhi
bidhaa zinazouzwa na Taasisi hiyo wadau waliochangia matibabu ya watoto wenye
magonjwa ya moyo wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa
maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
Na: JKCI
********************************************************************************************************
Wananchi wamehimizwa
kujitokeza kuchangia gharama za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Rai hiyo imetolewa leo
na mjumbe wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Heart Team Africa Foundation (HTAF)
Irene Mbonde wakati wa maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa.
Irene alisema Taasisi
hiyo ni mara yake ya kwanza kushiriki katika maonesho ya Sabasaba wakiwa na
lengo la kuitambulisha taasisi hiyo katika jamii pamoja na kukusanya fedha za
matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo.
“Hadi sasa kupitia
maonesho haya tumeshakusanya shilingi Milioni 1,566,400/= kwaajili ya kuchangia
matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI)”, alisema Irene
Irene alisema sambamba
na fedha hizo pia amejitokeza mdau mmoja ambeye ameahidi kuchangia gharama za
matibabu kwa watoto 10 wenye magonjwa ya moyo wanaotibiwa na JKCI baada ya
kumalizika kwa maonesho hayo.
Irene alisema mwitikio
wa kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto umekuwa mzuri kwani kila anayefika
katika banda hilo anaguswa kuchangia na kwa wale ambao hawakuwa wamejiandaa
wameahidi kushiriki kuchangia kwa wakati mwingine.
“Uchangiaji wa matibabu
ya moyo kwa watoto unaofanywa katika banda letu ni pamoja na kununua bidhaa
mbalimbali tulizonazo na wengine wamekuwa wakichangia fedha taslim”,
“Tunaendelea kuwakaribisha
watu wengine ambao hawajafika katika banda letu kututembelea na kuendelea
kuwachangia watoto wenye magonjwa ya moyo ambao wanatoka katika familia
zisizokuwa na uwezo wa kugharamia matibabu yao”, alisema Irene
Kwa upande wake mdau
aliyechangia fedha za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo ambaye hakutaka
jina lake lifahamike alisema familia nyingi za kitanzania zina uwezo wa kati
hivyo wakikutana na changamoto za magonjwa makubwa kama vile ya moyo wanakuwa
katika wakati mgumu na upoteza tumaini.
“Kwakweli
nimefurahishwa kuiona taasisi hii inafanya jambo la kipekee kuwasaidia watoto
wanaohitaji msaada wa matibabu, huu ni mfano wa kuigwa”. Alisema mdau huyo
Mdau alisema jamii
inapaswa kuiunga mkono Taasisi hiyo kuhakikisha watoto wenye magonjwa ya moyo
na magonjwa mengine makubwa wanaotoka katika familia duni wanapata matibabu kwa
wakati na kwa urahisi.
Taasisi ya Heart Team
Africa Foundation (HTAF) ni taasisi isiyo ya Kiserikali inahusika na kutafuta
fedha kwaajili ya kugharamia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo
wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wa kugharmia matibabu ya moyo
wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Comments
Post a Comment