JKCI kuwajengea uwezo wataalamu wa Hospitali ya Benjamini Mkapa
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi wakikabidhiana hati ya makubaliano ya ushirikiano wa matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi. Makubaliano hayo yalisainiwa jana katika Hospitali ya Benjamini Mkapa iliyopo jijini Dodoma.
***************************************************************************************************************************************************************************************************************************************
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa matibabu ya ubingwa bobezi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia uwezo wa wataalamu wa ndani ya nchi.
Makubaliano hayo yalisainiwa jana katika Hospitali ya
Benjamini Mkapa (BMH) iliyopo jijini Dodoma na Wakurugenzi watendaji wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na BMH.
Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alisema ni jambo la kupendeza kuona
wataalamu waliopo ndani ya nchi wanasaini makubaliano ya kujengeana uwezo wao
kwa wao na kutotegemea wataalamu kutoka nje ya nchi.
Mhe. Mhagama alisema siku za nyuma walikuwa wanawategemea
wataalamu kutoka nje ya nchi kuja kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani ya nchi
lakini sasa hivi mambo yamebadilika wataalamu wa ndani wanajengeana uwezo wao
kwa wao na kuna wataalamu wanatoka nje ya nchi wanakuja kujengewa uwezo hapa
nchini.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika majengo, vifaa tiba vya
kisasa na kusomesha wataalamu wa afya kitu kilichosababisha huduma za matibabu
ya ubingwa bobezi kupatikana hapa nchini”, alisema Mhe. Mhagama.
Aidha Waziri huyo wa Afya alisema kutokana na uwekezaji
mkubwa uliofanyika katika sekta ya Afya na Tanzania kupokea wagonjwa kutoka nje
ya nchi ambao wanakuja kutibiwa, wakati umefika sasa kwa Hospitali zinazotoa
huduma za ubingwa bobezi kuimarisha Utalii Tiba na kuhakikisha wanatoa huduma
bora kwa kufuata miongozi ya afya kwa wagonjwa wanaowahudumia.
“Nimepokea ripoti ya kambi maalumu ya matibabu iliyofanyika
Visiwani Comoro ambayo ilishirikisha wataalamu kutoka JKCI, BMH, Hospitali ya
Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na Taasisi
ya Saratani Ocean Road, ninawaomba muendelee kuungana kwa pamoja kama mlivyofanya Comoro muende
katika nchi nyingine kutoa huduma za ubingwa bobezi ili wale mtakaowakuta na
shida waje kutibiwa hapa nchini”,alisema Mhe. Jenista.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema ushirikiano uliokuwepo baina yao na
BMH umesaidia kuimarika kwa upatikanaji wa huduma ya matibabu ya moyo hapa
nchini.
“Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete wamekuwa
wakiwajengea uwezo wataalamu wa magonjwa wa moyo waliopo BMH kwa kufanya hivi
upatikanaji wa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo umeongezeka na kuwafikia
wananchi wengi zaidi kwa uharaka”, alisema Dkt. Kisenge.
Akikabidhi taarifa ya kambi maalumu ya matibabu ya ubingwa
bobezi wa magonjwa mbalimbali iliyofanyika Visiwani Comoro Dkt. Kisenge ambaye
alikuwa mratibu wa kambi hiyo alisema waliona zaidi ya wagonjwa 2700 na
wagonjwa zaidi ya 400 walishafika hapa nchini kutibiwa na wameingiza zaidi ya
shilingi bilioni 2.
“Mwishoni mwa mwaka jana tulienda Visiwani Comoro kuwatibu
wenzetu ambao wanatutegemea Tanzania kupata huduma za ubingwa bobezi, tukiwa nchini
humo tuliwajengea uwezo wataalamu wao na kujenga ushirikiano baina ya hospitali
zao na zetu”, alisema Dkt. Kisenge.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa
(BMH) Prof. Abel Makubi alisema ushirikiano wa BMH na JKCI ulianza miaka mingi
iliyopita lakini sasa hivi wameona wauweke katika maandishi.
“Tutaendelea
kushirikiana katika kufanya tafiti za magonjwa ya moyo, kutoa mafunzo kwa
wataalamu wetu na kubadilishana ujuzi wa kazi hii ikiwa ni pamoja na kufanya
matibabu ya pamoja”, alisema Prof. Makubi.
Katika hafla hiyo ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo ilikwenda sambamba na uzinduzi wa kliniki ya wagonjwa wa kimataifa, wagonjwa maalumu na uchunguzi wa afya katika Hospitali ya Benjamini Mkapa Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama alimteua Dkt. Peter Kisenge Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Utalii Tiba nchini.
Comments
Post a Comment