ALMC na MOI kuendesha kambi maalumu ya matibabu ya magonjwa ya mifupa Arusha

 Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya mifupa na mishipa ya fahamu itakayofanywa na wataalamu wa  Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) ambayp inayosimamiwa na JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) Antony Assey akielezea huduma ambazo Taasisi hiyo itazitoa wakati wa kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya mifupa na mishipa ya fahamu itakayofanyika tarehe 23-27/02/2026 katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mkutano na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya siku 5 ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali ya mifupa na mishipa ya fahamu itakayofanywa na wataalamu wa Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) inayosimamiwa na JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI).

**********************************************************************************************************************************************************************************

Wakazi  wa Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifupa na mishipa ya fahamu katika Hospitali ya Arusha Medical Center (ALMC) iliyopo jijini Arusha inayosimamiwa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Rai hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katik ukumbi wa JKCI uliopo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Waane ambaye pia ni Dakari bingwa wa magonjwa ya moyo na mtaalamu wa kuzibua mishipa ya damu ya moyo iliyoziba alisema katika jitihada za serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi, JKCI kwa kushirikia na Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) watafanya uchunguzi wa magonjwa ya ubongo, mifupa, uti wa mgongo,majeruhi na mishipa ya fahamu.

“Kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wenye maumivu ya mifupa katika kanda ya kaskazini kwa watoto na watu wazima, kwa kufanya kambi hii ya siku tano ambayo itafanyika bila gharama tunatarajia kuwafanyia uchunguzi wagonjwa zaidi ya 200 kwa siku” alisema Waane.

“Hospitali ya ALMC ambayo sasa ipo chini ya JKCI imekuwa ikitoa huduma za matibabu ya magonjwa ya mifupa kwa muda mrefu kwa kushirikiana na MOI tuna uhakika wakutoa matibabu ya kibingwa na kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata matibabu hayo jijini Dar es Salaam” alisema Dkt. Waane.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) Dkt. Anthony Assey alisema watalaamu wa magonjwa ya mifupa, mishipa ya damu na uti wa mgongo watatoa huduma katika Hospitali ya ALMC ili kupunguza matatizo ya maumivu ya shingo, mgongo na kiuno ambayo yamekuwa wakiwasumbua watu wengi.

“Tunalenga kutoa huduma za kibingwa na hata upasuaji kwa watu ambao walipata ajali wakapona lakini ajali ziliwapelekea kupata ulemavu pamoja na huduma za magonjwa ya ubongo” alisema Dkt. Assey.

Dkt Assey amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center (ALMC) ili watambue hali zao za kiafya na kupatiwa matibabu ya kibingwa.

“Mbali na huduma hizi tunazozitoa, wananchi wanatakiwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kama kufanya mazoezi na kuzingatia ulaji unaofaa, kwani kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wenye uzito uliopita kiasi ambao unaweza kuwasababishia kupata matatizo ya kiafya” alisema Dkt Assey.

Comments

Popular posts from this blog

JKCI na Burkina Faso zasaini makubaliano ya ushirikiano katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo

Wanawake waaswa kulinda mioyo yao, kuepuka sukari na chumvi kupita kiasi

Msumbiji kushirikiana na JKCI katika tiba ya moyo